Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga amewashauri wananchi kufuata na kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo ili kuweza kufanya kilimo chenye tija.
Mhe. Taraba ametoa ushauri huo leo wakati akikagua shughuli mbalimbali za kilimo katika kijiji cha Negezi kilichopo kata ya Ukenyenge wilayani humo.
Akikagua shughuli za uvunaji na umenyaji karanga zilizovunwa katika shamba darasa lake alisema kama wananchi watazingatia kanuni za kilimo zinazotolewa na wataalamu watapata mazao mengi.
“Kama unavyoona hapa kama ambavyo tuliagizwa ila mtumishi awe na shamba darasa name nimelima japo ni eneo dogo tu la shamba lakini nimeweza kuvuna karanga nyingi hii ni kwasababu nimefuata ushauri wa wataalamu,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa wananchi wazingatie uchaguzi bora wa mbegu ambazo zitaweza kuota kwa muda mfupi na hatimaye kustawi na kutoa mazao kwa wingi.
Aidha aliwashauri kutumia viuatilifu ili kuua wadudu wanaoshambulia mazao yakiwa shambani ili kuepuka hasara wanayoweza kuipata na kushindwa kuvuna kama inavyopaswa.
“Mimi hapa nilizingatia ushauri wa wataalamu wa kililo nilipalilia shamba langu na magugu hayakuweza kupata nafasi na pia nilipanda kwa nafasi na nimeona matunda katika kilimo nilichofanya,” alisisitiza.
Mhe. Taraba pia alitumia nafasi hiyo kuwashauri watumishi wengine hasa wa sekta ya kilimo kuwa na mashamba darasa kwa wingi ili wananchi wapate kujifunza na kujikomboa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa