Kaimu Meneja Tanesco Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhandisi Khamis Mbembe akielezea mkakati wa miradi mbalimbali ya uunganishaji umeme kwa wananchi wa Kishapu ifikapo 2025 vijiji vyote viwe vimepata huduma hiyo leo alipokuwa kwenye baraza la madiwani la uwasilishwaji taarifa za Kata leo Mei,8,2024 katika ukumbi wa Halmashauri
Madiwani wa Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamesikitishwa na kasi ya usambazaji umeme,maji na ukarabati wa miundombinu ya barabara suala linalopelekea wao kupokea maswali mengi kutoka kwa wananchi wanaowawakilisha.
Wakihoji maswali kuhusiana na kero hizo leo Mei,8,2024 katika baraza la Madiwani la uwasilishwaji taarifa za Kata lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wawakilishi wa kata za Kishapu, Shagihilu,Mwakipoya,Somagedi,Itilima,Ndololeji pamoja na Ngofila wamesema miradi ya umeme inasuasua katika uwekaji nguzo na hata kucheleweshwa usambazaji kwa wateja ambao ni wananchi.
Diwani wa Kata ya Itilima Mhe. Lameck Subata amesema kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo Tanesco wanatakiwa wahakikishe wanasogeza huduma kwa haraka ni pamoja na taasisi zote za serikali ikiwemo Zahanati na mashuleni.
Akijibu maswali ya madiwani Kaimu meneja Tanesco Wilaya Mhandisi Khamis Mbembe amethibitisha kucheleweshwa kwa ukamilishwaji wa miradi hiyo hivyo watahakikisha wanasimamia vyema mkandarasi ambaye wanae (Suma JKT) ahakikishe anaongeza kasi ya utekelezaji miradi hiyo huku akiwahakikishia wateja wa majumbani kwa atakehitaji kusogezewa huduma ya umeme ndani ya siku tatu(3) anapewa namba ya malipo kisha kuunganishiwa huduma hiyo muhimu.
Aidha akijibu maswali ya madiwani waliohoji kuhusu uunganishwaji wa maji kutoka Ziwa Victoria katika maeneo ya Seseko,Mpumbula,Bubiki,Bunambiyu,Mwamalasa pamoja na maeneo mengine ya Wilaya Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Kishapu Mhandisi Dickson Kamazima amesema Mamlaka inaendelea na utatuzi wa changamoto hizo huku baadhi ya maeneo hatua za awali tayari zimekamilishwa na maeneo mengine wanaendelea na taratibu zingine kwa mujibu wa sheria kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi.
"Waheshimiwa ni kweli huduma hii ni muhimu na Ruwasa inahakikisha inafanya bidii kwa kuandikia maandiko kwenye miradi inayohitaji fedha nyingi ukiwemo mradi wa Mwabusiga,na kwa Mwamalasa tayari hii leo tumempeleka Local fundi kwa ajili ya kuanza hatua za awali na vifaa vipo ofsini,kwa Masanga-Ndololeji tunasubiria maji yapungue kwenye chanzo cha mto kisha mwezi wa nane tunaanza kushughulikia na pia kwa kushirikiana na Ijumaa hii tarehe 10,2024 kwa kushirikiana na KASHWASA tunaunganisha katika kijiji cha Seseko,Mpumbura", amesema Mhandisi Kamazima.
Kaimu Meneja TARURA Wilaya ya Kishapu Mhandisi Hussein Shaweji akijibu maswali ya madiwani kuhusiana na ubovu wa miundombinu ya barabara nyingi za Wilaya kutopitika na zingine kupitika kwa shida huku zikitegemewa kuwa sababu ya kukuza mapato ya Halmashauri amesema tayari wameshafanya upembuzi yakinifu tangia Novemba hadi Februali mwaka huu na baadhi ya barabara zinaendelea na ukarabati.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa