Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mwanamke hivyo inaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya.
Kengese amesema hayo Machi 8 wakati akizungumza na wananchi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kiwilaya kwenye kata ya Songwa ambapo washiriki shughuli za ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya unaondelea.
Alisema kukamilika kwa kituo cha afya cha Songwa kutasaidia kusogeza karibu huduma za afya zikiwemo ya upasuaji kwa wajawazito watakaokuwa wanahitaji huduma ya upasuaji.
“Hapa kwenye kata ya Songwa kuna kazi inayofanyika katika kituo hiki cha afya ili kukipa hadhi ya kutoa huduma za upasuaji hali itakayosaidia kusogeza huduma karibu zaidi hivyo wajawazito watakaohitaji upasuaji wataipata huduma hiyo,” alisema.
Katibu Tawala aliongeza kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutambua mchango wa mwanamke na kuthamini jitihada zake katika shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Hivyo alisema kaulimbiu ya mwaka huu kuwa ‘Kuelekea Uchumi wa Viwanda Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini’ inaakisi namna mwanamke anavyotambuliwa katika sekta hii.
Alisema usawa wa kijinsia utawezesha wanawake kupata ajira na kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo katika familia na Taifa kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa