Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewaagiza maafisa ugani wa kata zote kuhakikisha wanawafikia wakulima na kuwafundisha mbinu bora za kilimo chenye tija.
Ameagiza pia wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame hususan mtama na uwele badala ya kuwa na kasumba ya kung’ang’ania kilimo cha mahindi ambacho katika sehemu kubwa ya wilaya hakifanyi vizuri.
Taraba alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake kwenye mashamba ya mtama katika kata za Uchunga, Mwaweja na Ukenyenge kujionea na kufanya tathmini ya kilimo wilayani humo.
Aliwataka maofisa hao kujiwekea utamaduni wa kutembelea mashamba ili kuwafundisha namna ya matumizi ya mbegu bora kwani wengi wao hupanda bila utaalamu.
Aliwataka kusimamia Sheria ndogo ya mwaka 2008 ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inasisitiza kuwa kila kaya wilayani humo iweze kulima ekari mbili za mazao yanayostahili ukame ambayo ni mtama.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa hata hivyo wakulima wengi wilayani humo wameweza kutekeleza sheria ndogo hiyo lakini wamepata changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maarifa ya matumizi ya aina sahihi za mbegu.
“Ziara hii imetufundisha mambo mengi kwa mfano shambani hapa tumeshuhudia wakulima hawa wametumia mbegu za aina tano tofauti katika shamba moja sasa kama wangepata elimu wangetumia mbegu za aina moja zisizoshambuliwa na ndege.
”Hivyo naagiza wataalamu wa kilimo wahamie mashambani kufundisha wakulima na wawe na mashamba darasa yawe mfano wa kujifunzia wananchi nao waige na kusonga mbele,” alisisitiza Taraba.
Aidha, alipiga marufuku wakulima kuuza wa mazao kwa ajili ya matumizi mengine pasipo kujiwekea akiba na kuonya atakayefanya hivyo atachuliwa hatua kali ikiwemo kupigwa faini.
Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya alionya kuwa wapo baadhi ya wakulima wana tabia ya kufanya biashara ya mtama kwa ajili ya kutengeneza pombe huku wao wakibaki bila ya chakula.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mkulima wa mtama katika Kata ya Mwaweja, Mariam Nkinga kwa niaba ya wenzake aliomba Serikali iwapelekee mbegu fupi zinazokua kwa haraka.
Alisema wanapata changamoto ya mtama wao kuliwa na ndege aina ya kwelea pamoja na wadudu ukiwa shambani kutokana na mbegu wanazotumia kuchelewa kukomaa na hivyo kukaa muda mrefu shambani.
Nkinga alioimba wataalamu wawe wanapita mara kwa mara kunyunyizia dawa mazalia ya wadudu na ndege waharibifu wa mazao ili wasiweze kuzaliana na kufika mashambani.
Aliwashauri wananchi kulima zao la mtama kwa wingi na kuacha kasumba ya kuchagua chakula na kulima mahindi ambayo matokeo yake hawastawi yanakufa kutokana na ukame.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa