Mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa Kamati ya kuvunjika kwa kingo za bwawa la maji tope katika mgodi wa uchimbaji madini ya almasi wa Williamson Diamond Limited uliopo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Joseph Modest Mkude amefanya kikao na uongozi wa mgodi huo ili kufahamu hatua ya ulipaji wa fidia waliyofikia tangu kupasuka kwa bwawa hilo. Katika Kikaoo hicho ameambatana na Wajumbe wa Kamati hiyo
Akitoa taarifa wakati wa kikao hicho, Afisa Uhusiano wa mgodi huo ndugu Benard Mihayo amesema tayari timu yao imeshafanya tathimini na kubaini waathiriwa wanaostahili kulipwa fidia na kujengewa nyumba kufuatia tope la mgodi huo kuharibu makazi na mashamba ya wakazi wa Vijiji vya Ng'wanholo na Nyenze vilivyopo Kata ya Mwadui Luhumbo kwa kufunikwa na tope mnamo Novemba 7, 2022.
“Tathimini imefanyika na kubaini makundi yanayostahili kulipwa fidia kuwa ni pamoja na wamiliki wa ardhi, wapangaji, waliokuwa wamekodisha mashamba pamoja na waliopoteza mifugo na tayari tumeanza ulipaji wa fidia na mpaka sasa ulipaji upo Asilimia 18 na wahanga wengine tunaendelea kuwafungulia akaunti za benki ili tuweze kuwalipa stahiki zao,” alisema Mihayo.
Kwa upande wake Meneja wa mgodi wa Mwadui, Ayoub Mwenda ameishukuru tume ya madini na Serikali kwa kuendelea kuwapa ushirikiano katika kuhakikisha waathiriwa wote wanalipwa fidia kwa kuzingatia sheria na miongozi ya Serikali.
“Tunaishukuru tume ya madini kwa kuendelea kushirikiana nasi ambapo Machi 6 mwaka huu tumepata kibali cha kuendelea kujenga bwawa jipya la Tope hadi sasa ujenzi umefika asilimia 25 na kufikia Julai 2023 tutakuwa tumekamilisha na uzalishaji kuendelea," alisema Mwenda.
Aidha, Mhe. Mkude ameupongeza uongozi wa mgodi huo kwa hatua waliyofika na ameahidi kutoa ushirikiano kila muda kuhakikisha waathirika wa tope wanapata stahiki zao
“Jitahidini kulisukuma kwa haraka ili waathiriwa waliobakia wapate fidia kufikia 31 Machi 2023 Wahanga wote wawe wameshalipwa na mimi nitashirikiana nanyi kila mkihitaji msaada kutoka ofisini kwangu," alisema Mhe. Mkude.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa