Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe.Joseph Mkude, amezindua zoezi la uwekaji Alama kwenye mipaka ya vyanzo vya maji katika Mabwawa ya Songwa na Mhumbu wilayani humo ili kuvilinda vyanzo hivyo vya maji kwa kuzuia shughuli za kibinadamu.
Zoezi hilo la limefanyika jana likiambatana Sambamba na upandaji miti, ambalo limeratibiwa na Bodi ya Maji Bonde la Kati.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya kuzindua uwekaji wa Alama hizo, Mhandisi wa Mazingira kutoka Bodi ya Maji Bonde la Kati Nyacheli Mramba, amesema wameweka Alama hizo za mipaka na Mabango ili kuzuia wananchi wasifanye shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo ili kuvilinda visitoweke.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, ametoa wito kwa wananchi wasifanye shughuli za kibinadamu kwenye Mabwawa hayo, ikiwamo na kufanya shughuli za kilimo na uchimbaji madini, bali wavitunze vyanzo hivyo vya maji kwa faida yao na vizazi vijavyo.
“Natoa wito kwa wananchi vitunzeni vyanzo hivi vya maji msifanye kabisa shughuli za kibinadamu, na katika Mabwawa haya yamejengwa Matangi kwa ajili ya kunyweshea mifugo yatumieni na msiingize tena mifugo ndani ya maji,”amesema Mkude.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi wa Kishapu kuzitumia ipasavyo Mvua ambazo zinanyesha hivi sasa, kwa kupanda miti ili kuifanya Kishapu kuwa ya kijana.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Songwa, wamesema uwekaji huo wa Alama za mipaka katika Mabwawa hayo,utasaidia kuvilinda vyanzo hivyo vya maji ambavyo vilikuwa hatarini kutoweka, kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwamo kilimo, uvuvi na uchimbaji madini.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa