Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabanga Taraba amezindua kampeni ya umezaji dawa za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa watoto wa miaka minne hadi 15.
Katika uzinduzi huo uliofanyika shule ya masingi Mhunze aliwataka wazazi kuacha dhana potofu ya kuwazuia watoto kupata kinga ya magonjwa mbalimbali yakiwemo minyoo na kichocho mashuleni.
Alisema kuzuia magonjwa ni jambo muhimu ili kulinda afya hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto inafanya kampeni hiyo ili kulinda watoto dhidi ya magonjwa hayo.
“Serikali inajua hakuna taifa kama watu wake hawana afya na ndiyo maana imetumia fedha na muda ili kuhakikisha watu wake wanakuwa na afya na hapa mtoto analindwa ili akiwa mtu mzima awe na afya,” alisisitiza.
Aliwahimiza wazazi wajenge utamaduni wa kuwapeleka watoto kwenye vituo vinavyotangazwa kutoa chanjo mbalimbali vikiwemo mashuleni wapate dawa huku akisisitiza kufuata masharti ya madaktari.
Alikemea tabia ya baadhi ya wazazi kukatalia watoto wao kupata dawa kwa sababu zao mbalimbali na kuwataka watoe ushirikiano ili wakingwe na magonjwa.
Taraba aliongeza kuwa kampeni hiyo ni muendelezo na kuwa wilaya hiyo tangu mwaka 2016 imeweza kutokomeza magonjwa mengine ya aina hiyo ukiwemo trakoma.
Kampeni hiyo inayofanyika katika shule zote 122 za wilayani Kishapu inatarajiwa kuwafikia watoto wote wakiwemo walioandikishwa shuleni na wasiyoandikishwa.
Kampeni hiyo inafanyika kwa lengo la kuhakikisha kiwango kinapungua kabisa cha magonjwa hayo kufikia mwaka 2020 ambayo ni pamoja na trakoma, usubi, matende na ngirimaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga alishukuru na kupongeza zoezi hilo linaloendeshwa kwa watoto hao.
Alisema kuwa itasaidia kuimarisha afya za watoto hao wa shule na kuwa watakuwa na wasaa wa kusoma vizuri na hivyo kuweza kufaulu katika masomo yao.
“Niwashukuru walioandaa zoezi hili kwani sasa magonjwa yaliyokuwa hayatiliwi maanani sasa yameanza kupewa kipaumbele na mimi naamini zoezi hili litaendelea kila mwaka,” alisema Magoiga.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa