Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Stephen Magoiga amesema kuundwa kwa mfumo wa sekta za umma (PS3) utasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku zinasimamiwa vizuri.
Amesema mfumo huo pia utaleta tija katika vituo vya kutolea huduma na kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi katika mahesabu ya mapato na matumizi ya halmashauri nchini.
Magoiga ametoa kauli hiyo wilayani hapa wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma (FFARS) yaliyofanyika katika kata ya Maganzo.
Alisema mafunzo hayo yaliyolenga waratibu elimu kata na watoa huduma katika vituo vya afya yatawajengea uwezo wa kusimamia taarifa za matumizi ya fedha na kuhakikisha zinatolewa kwa usahihi, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Nafahamu kwamba kwamba mafunzo haya yanafanyika sehemu mbalimbali nchini ili kuhakikisha mnakuwa katika nafasi ya kwenda kuwafundisha watoa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za elimu vikijumuisha zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule za sekondari na za msingi,” alifafanua.
Magoiga aliongeza kuwa lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinakuwa na mfumo maalumu wa kuandaa taarifa za mapato na matumizi hivyo kuchangia uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alikiri changamoto ya upatikanaji taarifa sahihi za fedha vituoni hivyo halmashauri kushindwa kutoa taarifa sahihi za matumizi ya ruzuku zinazotolewa na wakati mwingine kusababisha kupata hati ya mashaka kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Ukweli ni kwamba hakukuwa na mfumo sahihi wa kusaidia kulizuia hilo lakini kwa mfumo huu mpya sasa, utasaidia kuhakikisha kunakuwa na muundo maalum wa kuhifadhi taarifa za mapato na matumizi, na hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji wa vituo hivyo kupunguza changamoto zilizokuwepo awali,” alisema.
Aidha mkurugenzi huyo aliagiza matumizi ya tovuti za mikoa na halmashauri katika kuweka taarifa zote za mapato na matumizi ya fedha za umma ambayo ni maagizo ya Serikali.
Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wizara mama zinazoshughulikia sekta za fedha, afya na elimu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa