Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na Shirika la Misaada ya Kijamii (REDESO)/OFXAM imetoa msaada wa vifaranga vya samaki 10,000 vyenye thamani ya sh. milioni 3 kwa kikundi cha ufugaji samaki.
Msaada huo umetolewa kwa kikundi hicho katika kijiji cha Lubaga ulipo mradi huo na Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo.
Akikabidhi msaada huo Kengese aliwataka wanakikundi hao kuendeleza na kuutunza mradi huo kwani utakuwa ni mkombozi kwa kijiji hicho na wilaya kwa ujumla katika kuimarisha kipato chao na afya za wananchi kwa kupata kitoweo cha samaki.
Aliishukuru REDESO/ OXFAM kwa kutoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 5 kwa ajili ya kuwekwa kwenye bwawa na Halmashauri iliyotoa vifaranga kwa ajili ya kupandikizwa bwawani.
Aliwataka kujiandaa na soko la samaki na kutumia maarifa waliyopewa na wataalamu wa uvuvi kutoka Halmashauri ili mradi huo uwe na tija.
“Ndugu zangu mmekabidhiwa mradi huu muutunze na itakuwa si vyema tena tukasikia mifugo imeingia humu kwenye bwawa na kunywa maji ma kuua samaki hawa, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwani sote tunatambua zimetumika gharama kubwa kuanzisha mradi huu,” alionya.
Afisa Mifugo na Uvuvi Wilaya, Dk. Alphonce Bagambabyaki aliwapa elimu ya utengenezaji chakula cha samaki kwa njia rahisi ili na kusema kuwa huu mradi sasa hivyo wa kwao hivyo wanapaswa kuuendeleza.
Alisisitiza kuwa Serikali na wahisani zimetoa msaada wa vifaa vya bwawa na vifaranga vya samaki hivyo wao kama kikundi cha wafugaji wanapaswa kuwajibika kuandaa chakula.
Pia aliwataka kuufanya mradi kuwa ni wanakijiji wote na si wa kikundi hicho tu na kuwa wafungue milango kwa ajili ya wengine kujiunga ili waweze kuunganisha nguvu na kuendeleza vyema mradi huo.
Mradi huo wa bwawa la ni moja ya mikakati ya Kishapu kuwa sehemu maarufu ya samaki na samaki hao wanatarajiwa kuanza kuvuliwa baada ya kipindi cha miezi minane na hivyo kupunguza upungufu wa kitoweo.
Pia katika shughuli hiyo kulifanyika zoezi la upandaji miti katika eneo hilo kama ambavyo Mkuu wa wilaya, Mh. Nyabaganga Taraba alivyozindua Novemba 22 na Katibu Tawala alitumia nafasi hiyo kushiriki kupanda miti.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa