Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inatarajiwa kuongeza huduma nyingine ya upasuaji baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo la upasuaji katika kituo cha afya kilichopo kata ya Songwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Mipango katika Halmashauri hiyo, kituo hicho kilitenga jumla ya sh. milioni 400 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu yake.
Gharama za ujenzi wa jengo la upasuaji zinatarajiwa kuwa sh. milioni 78.3, maabara sh. milioni 54 jengo la mama na mtoto sh. milioni 88.3 pamoja na chumba cha kuhifadhi maiti sh. 24.4 ambapo jumla sh. milioni 291 zimeanza kutumika.
Inaelezwa kuwa sh. milioni 108.9 itakayobaki itatumika kukamilisha miundombinu ya kituo hicho cha afya ikiwemo ya maji, kichomea taka na ujenzi wa shimo la kutupa kondo la nyuma.
Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kusogeza karibu zaidi huduma ya upasuaji ambayo wananchi hao walilazimika kuipata katika vituo vingine vya afya vilivyopo mbali au Hospitali ya Wilaya.
Miradi hii ya maendeleo pia inachangiwa kwa kiasi na nguvu kazi ya wananchi ambapo mara kwa mara Serikali imekuwa ikiwahamasisha waione kuwa ni yao na si tu kuiachia Serikali kwa asilimia zote.
Pamoja na jitihada hizo za Serikali katika kuboresha huduma zake kumekuwepo na changamoto zinazoukabili mradi huo zikiwemo uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu kujitolea nguvu kazi.
Wananchi wanaelezwa kutokuwa na uelewa wa dhana ya ushirikishaji wa jamii katika masuala ya miradi ya maendeleo huku wengine wakiamini ni Serikali pekee ndiyo itakafanya shughuli zote.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa