Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wamefanya maandamano ya amani kwa kupita katika mitaa mbalimbali ndani ya Halmashauri ya wilaya hiyo wakiwa na mabango yenye jumbe tofauti tofauti za kuhamasisha kupinga ukatili wilayani humo.
Maandamano hayo yamefanyika leo Desemba 4, 2020 ambapo Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wamekutana na kufanya maandamano hayo kuanzia eneo la Mto Tungu hadi Shule ya Sekondari Kishapu ikiwa ni nyenzo moja wapo katika maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Miongoni mwa wadau walioshiriki maandamano hayo ni Shirika lisilo la Kiserikali la REDESO, NMB, Red Cross, TCRS, Ustawi wa Jamii pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambao kwa sauti moja wameihimiza jamii kuacha ukatili kwa kuwa madhara yatokanayo na ukatili yanaathari kubwa kiafya, kisaikolojia, kiuchumi na kimwili na kusema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo hivyo basi jamii haina budi kuachana navyo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kishapu ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Rose Mbwambo amesema maadhimisho hayo ya kupinga ukatili yanaakisi umakini wa Dawati hilo katika kutoa elimu ya haki na uwajibikaji ili kupinga ukatili wa kijinsia na kwamba dawati hilo limekuwa likifanya kazi kwa weledi ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanaume 9 wamefungwa kifugo cha miaka 30 kila mmoja.
”Ukitazama takwimu zaJanuari hadi Novemba, 2020 tumepata taarifa 91 za ubakaji, kati ya hizo taarifa watu 43 wamefikishwa mahakamani na taarifa hizo ziko katika hatua ya ufuatiliaji, watu 9 wamepatikana na hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela na kesi 24 zipo katika hatua ya upelelezi. Changamoto iliyopo ni ushirikiano duni unaotolewa na walengwa pamoja na mashahidi wanaofanya mapatano ya kifamilia na kumaliza kesi za namna hiyo, lakini dawati linaendelea kuchukua hatua za kisheria ulikuendelea kubaini makosa hayo”amesema Rose.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba ambaye aliyapokea maandamano hayo amesema msimamo wa serikali ni kuhakikisha hali ya usawa, utulivu na amani katika kuvikabili vitendo vyote vinavyokiuka haki za binadamu na kuitaka jamii kuacha imani za kishirikina jambo linalowaweka watoto kwenye hatari ya kubakwa pia kundi la wazee kuwa katika hatari ya mauaji.
“Wilaya ya Kishapu sio kwamba imeharibiwa na mila na desturi bali ni uelewa wa baadhi ya wazazi kutokutambua majukumu yao katika malezi ya motto na mchango wa motto hasa wa kike kwenye maendeleo lakini imani za kishirikina zimekuwa mwiba unaochoma kwani watoto wanakuwa na hofu ya kubakwa na kulawitiwa pia wazee kuingiwa na hofu ya kuuawa” alisema Taraba.
“Lakini Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo tunaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuhakikisha tunachukua hatua kali za kisheria kwa wale wanaoendelea na vitendo hivyo kwa sababu zao, hatutawafumbia macho” ameongeza Taraba
Maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatil iyalioongozwanaDawati la Jinsia na Watoto wilayani Kishapu yalihitimishwa kwa ugawaji wa taulo za kike, madaftari, kalamu pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa pete kati ya Askari Polisi na wanafunzi wa shule ya sekondari Kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa