Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kutokomeza vitendo vya uhalifu katika maeneo yao.
Sirro ametoa mwito huo Februari 20, 2019 wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga wakati akizungumza na maafisa wa Polisi, viongozi mbalimbali na wananchi alipofanya ziara ya siku moja.
Pamoja na mwito huo, alisema Kishapu kwa sasa haina matukio makubwa ya kiuhalifu tofauti na zamani akieleza kuwa ni kutokana na umoja na ushirikiano baina Jeshi la Polisi na wananchi.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kutokomeza uhalifu unaanzia katika ngazi ya familia ambapo aliwataka wazazi kutoa taarifa pindi waonapo watoto wao wanabadilika kitabia.
“Wewe mzazi au mlezi unaona mtoto amebadilika ameanza kuvuta bangi husemi, tupeane taarifa zi walezi ukiona anabadilika tupeane taarifa siku zote information is power na tunafanikiwa kwa sababu ya taarifa,” alisisitiza IGP Sirro.
Katika ziara hiyo ambapo pia alitembelea eneo jipya litakalojengwa makao makuu ya Polisi Wilaya ya Kishapu alitangaza operesheni kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokomeza mauaji ya kishirikina.
Alionya watu wanaojifanya waganga na kupiga ramli chonganishi ambazo huchangia mauaji hatua inayosababisha uvunjifu wa sheria akisema Jeshi halitasita kuwashughulikia kama wahalifu wengine.
Awali akimkaribisha, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Taraba aliwataka wananchi wote kushikamana na kukemea vitendo hivyo vya mauaji ya kishirikina.
Mhe. Taraba alisema watu wote wanaguswa na matukio hayo na kuwa hivyo wanawajibika kuyakemea kuanzia ngazi ya familia na akieleza kuwa wahusika wanafahamika.
“Ndugu zangu sijawahi kusikia mtu anatajirika kwa kuua bali anatajirika kwa kufanya kazi kwani nchi hii ina rasilimali nyingi, tuna madini tuna nguvu tunao wataalamu hivyo tunaweza kupata mali bila kuua wenzetu,” alisema.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa