Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Kamati ya Fedha, Ungozi na Mipango halmashauri ya wilaya ya Kishapu imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kata za Lagana, Itilima na Talaga.
Katika ziara hiyo wajumbe hao pamoja na wataalamu kutoka halmashauri walitembelea maendeleo ya ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Mwadulu iliyopo kata ya Lagana.
Wakiwa eneo hilo wajumbe hao kupitia kwa mwenyekiti wa halmashauri, Boniphace Butondo walipongeza juhudi za uongozi wa shule hiyo kwa ubunifu na kutumia vizuri fedha za Serikali.
Butondo aliwataka wanakamati ya shule kuendelea kuupa ushirikiano uongozi wa shule hiyo ili waendelee kushughulikia shughuli za maendeleo kupitia mpango wa elimu bure.
Kamati hiyo iliweza pia kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya msingi Lagana ambayo inajengwa kwa nguvu ya wananchi ambapo walihimiza waendelee kuchangia.
Ziara hiyo pia ijumuisha kata ya Itilima ambapo wajumbe na wataalamu hao walikagua ujenzi wa vyumba viwili vya darasa shule ya msingi Ipililo pamoja na kata ya Talaga ukarabati wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Nhobola.
Waliridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi huo ambapo walimpongeza afisa elimu ufundi, Moshi Balele kwa kufuatilia kwa ukaribu shughuli zote zinazoendelea.
Hiyo ni mojawapo ya ziara za kukagua miradi ya maendeleo zinazofanywa na kamati mbalimbali za Baraza la Madiwani katika halmashauri hiyo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa