Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na kukagua utekelezaji wa Ilani kwenye miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Mabala Mlolwa akiwa ameambatana na wajumbe wake aliipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa utekelezaji wa miradi.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ule wa nyumba ya watumishi wa afya katika zahanati ya Shagihilu.
Mradi huo uliyojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Benjamin Mkapa ukiwa na thamani ya sh. Milioni 82.6.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa umetekelezwa kwa kiwango kizuri.
Ziara hiyo pia ilipitia kikundi cha watu wenye ualbino ambao wanajishughulisha na mradi wa maji safi na salama ambao umefadhiliwa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani.
Mwenyekiti huyo aliipongeza Kishapu kwa hatua ya kutoa fedha hizo ambazo ni sehemu ya asilimia 10 inayotengwa kwa makundi mbalimbali huku akiitaka kufuatilia maendeleo ya mradi huo.
“Nawapongeza Halmashauri kwa kutoa fedha kwa walemavu hizo shilingi milioni sita si haba lakini Afisa Maendeleo ya Jamii uwe unafuatilia twende nao tuwe nao karibu watu wakiomba mkopo tusisubiri kusumbuka baadae lazima tuone zinafanya kazi na kurudishwa marejesho,” alisisitiza Mlolwa.
Kwa upande mwingine ilikagua kiwanda kidogo cha kuwekea thamani mazao cha mjasiliamali Mabela Masolwa mjini Mhunze wilayani humo ambapo alipongeza kwa kuunga mono juhudi za Serikali ya viwanda.
Alisema kiwanda hicho pamoja na kuunga mkono uchumi wa viwanda lakini pia kinazalisha ajira kwa vijana wa eneo hilo ambao wangeweza hata kujitumbukiza katika vitendo vya kihalifu.
Pia Kamati hiyo ikiwa katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaoendelea kujengwa katika kijiji cha Unyanyembe kata ya Uchunga, Mlolwa aliwataka wananchi wa eneo hilo kuitunza miundombnu ya maji.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa