Maji ni moja ya mahitaji na rasilimali muhimu kwa uhai wa binadamu, wanyama na mimea ambapo yanapatikana kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo vya asili na vya kutengenezwa.
Katika Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga vyanzo vikuu vya maji kwa wananchi wake ni pamoja na visima vifupi, virefu, mabwawa na miradi michache ya maji ya bomba.
Mahitaji halisi ya maji kwa sasa katika wilaya hiyo ni mita za ujazo 15,303 kwa siku, lakini kiasi cha mita za ujazo 7,860.7 tu ndizo zinazoweza kupatikana na kutumiwa na wananchi wake.
Kutokana na na changamoto ya uhaba mkubwa wa maji unaosababishwa na mvua inayonyesha kwa kiwango kidogo kwa sasa wakazi wake wananufaika na huduma hii kwa kiwango cha wastani wa asilimia 51.6 vijijini na asilimia 45 mjini.
Itakumbukwa kuwa kwa wastani inakadiriwa kuwa Wilaya ya Kishapu hupata mvua inayonyesha kwa kiasi cha milimita 450 hadi 900 kwa mwaka.
Hata hivyo, kwa kuzingatia lengo la Taifa la kuwafikishia wananchi wa vijiji asilimia 90 ya maji safi na salama ndani ya umbali wa mita 400 ya makazi yao ifikapo mwaka 2020, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikisha Serikali Kuu, wadau na wananchi imepunguza tatizo hilo.
Hivi karibuni ilianza kwa kasi ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji kwa mradi wake wa maji ya Ziwa Victoria ambao unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh. bilioni 1.16.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Stephen Magoiga anabainisha kuwa mradi huo ulianza mwishoni mwa Oktoba mwaka huu baada ya taratibu za manunuzi ya bomba kukamilika ambapo hadi sasa umefikia asilimia 80.
Kazi zilizofanyika na kukamilika ni pamoja na uchimbaji mtaro wa kulaza bomba umbali wa mita 23,256 ambalo lina kipenyo cha milimita 315 na urefu wa mita 23,256 pamoja na kuunganisha viungio mbalimbali vya bomba na ‘valve’ za kuondolea hewa.
Kwa mujibu wa Magoiga ni kwamba hadi sasa takriban sh. milioni 820 kimetumika kununua mabomba, viungio, dira za maji 1,500 pamoja na shughuli mbalimbali za mradi huo.
Bomba hilo limepitia katika vijiji 16 ambavyo kwa sasa havina huduma ya maji na yanaweza kuhudumia zaidi ya watu 45,000 hivyo Halmashauri inafanya jitihada za kutafuta fedha za kuyasambaza.
Mradi huu ni mwendelezo wa upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika Mji wa Kishapu kupitia Maganzo na Mgodi wa Almasi wa Mwadui.
Itakumbukwa ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji ulihusisha ulazaji wa bomba la maji lenye urefu wa kilomita 70.2 kutoka Old Shinynga na ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji lenye mita za ujazo 1,200 mjini Kishapu.
Hivi sasa kwa wananchi wa wilaya hiyo changamoto ya uhaba wa maji imeweza kutatuliwa kwa asilimia kubwa hali inayoweza kuchangia kuendelea kuimarika kwa uchumi.
Kwa maji safi na salama yanayopatikana kutoka chanzo cha Ziwa Victoria sasa wananchi wanaweza kufanya shughuli za maendeleo tofauti na ilivyokuwa nyuma ambapo walikuwa wakitumia muda mwingi kusaka maji.
Idara ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya Kishapu ikiongozwa na Mhandisi Lucas Said ambayo kwa sasa imezaa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira inaendesha mradi huo.
Awali ilikuwa ikisambaza maji kutoka chanzo kidogo cha maji kutoka Mto Tungu uliopo mjini Mhunze ambapo hata hivyo huduma hiyo ilikabiliwa na changamoto ikiwemo upungufu wa maji.
Kwa sasa baada ya kulifikisha bomba la maji kutoka chanzo cha ziwa hilo huduma ya maji imekuwa ya uhakika zaidi na saa za kufungulia maji zimeongezeka ikilinganishwa na awali.
Tayari tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni 1.2 limekamilika ambapo hivi karibuni katika ziara yake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Kakunda alikagua mradi huo.
Akizungumza akiwa kwenye mradi huo wa tanki la maji alipongeza juhudi za Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kahama-Shinyanga (Kashwasa) katika kuutekeleza.
Tanki hilo litakuwa likipokea maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza katika Mji wa Mhunze na vitongoji vyake na hivyo kuweza kutatua changamoto ya uhaba wa maji kama ilivyokuwa awali.
Halmashauri hiyo iko katika mikakati ya kuiomba Serikali Kuu kuisaidia fedha za kuzambaza maji hayo katika Mji wa Kishapu na vijiji vingine pamoja na kufanya usanifu na kujenga miundombinu ya majitaka.
Inaendeleza utafiti wa vyanzo vingine zaidi vya maji na kuyatumia ya ziwa hilo kuyasambaza vijiji vilivyopo jirani na bomba kuu. Pia kuelimisha jamii juu ya uchangiaji wa gharama za ujenzi, uendeshaji na ukarabati wa miundo mbinu ya maji.
Aidha, utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira katika vijiji 10 ulianza kwa mchakato wa kupata wataalamu washauri (consultants) wakisaidia kusanifu miradi, kutafiti maji ya ardhini na kusimamia kuchimba visima virefu na baadaye kuanza ujenzi wa miundombinu yake.
Programu hii ilijenga miradi ya maji katika baadhi ya vijiji kadri fedha ilivyokuwa ikipatikana na vilivyopewa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu kupitia awamu ya kwanza ya utekelezaji vilikuwa tisa.
Vijiji hivyo ni Nyenze, Iboja, Sekeididi, Mwigumbi, Mwamashimba, Bubinza, Mwamadulu, Idukilo na Bunambiyu ambapo jumla ya Sh. bilioni 3.5 zimetumika kuitekeleza kwa kuanzia usanifu hadi ujenzi wa miundombinu ya maji. Kwa pamoja miradi hiyo inahudumia wananchi takriban 24,750.
Mkakati wa Halmashauri
Katika mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri iliidhinishiwa kiasi cha Sh. bilioni 1.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira na hadi kufikia Novemba imeshapokea Sh. milioni 26 ambazo ni kwa ajili ya usanifu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi.
Utekelezaji wa Programu ya Maji awamu ya pili umeanza katika mwaka huu wa fedha kwa kuhusisha jumla ya miradi mitano katika vijiji vya Shagihilu, Ndoleleji, Lagana, Ikonongo na Unyanyembe.
Aidha, wakandarasi wako eneo la kazi (site) wakiendelea na ujenzi ambao uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na unaelezwa kuwa unatarajia kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.5.
Halmashauri hiyo pia imeweza kutekeleza mradi mwingine katika mji wa Maganzo ambao awali haukuwa na huduma ya maji hivyo kusababisha wakazi takriban zaidi ya 12,000 kutokuwa na uhakika wa huduma ya maji safi na salama.
Mji huu umefanikiwa kupata maji kutoka Ziwa Victoria kupitia ufadhili wa Shirika la Investing in Children and their Society (ICS) kwa gharama ya Sh. milioni 750. Ujenzi huo ulikamilika Machi 2017 na unahudumia wakazi wa Maganzo na kijiji cha Masagala.
Hata hivyo changamoto hazikosekani katika kutekeleza miradi ya maendeleo uhaba wa vyanzo vya maji vya kutosha na vya kuaminika unakabili utekelezaji wa mradi huo.
Mkakati uliopo ni Kuendeleza utafiti wa vyanzo vingine zaidi vya maji na kuyatumia maji ya ziwa Victoria na kuyasambaza vijiji vilivyopo jirani na bomba kuu
Pia uhaba wa fedha kwa miradi ya maji inayohitaji fedha nyingi unasababisha mradi kupata changamoto katika utekelezaji wake na hivyo wananchi kukosa huduma hiyo muhimu.
Elimu inaendelea kutolewa kwa jamii kuhusu ya uchangiaji wa gharama za ujenzi wa miradi hiyo na pia uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa