"Tunataka zawadi zinazotia moyo walimu na wamiliki wa shule katika Halmashauri ya Kishapu, tutoe zawadi zinazomotisha wadau wa elimu kama walimu ili kuwafanya watekeleze Majukumu yao kwa moyo mmoja. Hali kadhalika tuwapongeze wamiliki wa Shule ambao wameamua kuwekeza katika Elimu, wangeweza kuwekeza katika miradi mingine lakini wakaamua kujenga shule." Mkuu wa wilaya alisema.
Maneno hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Mheshimiwa Joseph Modest Mkude wakati akitoa hotuba ya kufunga kikao cha wadau wa Elimu leo katika Ukumbi wa Hotel ya Stage 2.
Katika kikao hicho cha wadau wa Elimu Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Kishapu mhe. Joseph Modest Mkude aliwataka Wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari kutoa taarifa zao za utekelezaji wa Majukumu katika sekta za Elimu kwa kueleza ufanisi na changamoto zinazosababisha Halmashauri ya Kishapu kutofanya vizuri katika taaluma lakini pia ufumbuzi wa changamoto hizo ili kuinua kiwango cha ufaulu katika shule za Msingi na Sekondari.
Kwa upande wao Wakuu wa Idara za Elimu Msingi na Sekondari kwa nyakati tofauti tofauti walieleza changamoto mbalimbali katika ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za kutwa kwa Shule za Sekondari kutokupata chakula cha mchana hivyo wanafunzi kukosa usikivu katika kujifunza, kusababisha wanafunzi kuwa na Msingi mbaya wa masomo haya tangu wakiwa vidato vya chini hali inayopelekea kuwa na ufaulu duni katika masomo yao, upungufu wa nyumba za walimu kwa shule za Msingi na Sekondari, upungufu wa miundombinu ya Elimu kama nyumba za walimu, walimu kuishi mbali na shule, uelewa ndogo wa dhana ya Elimu bure kwa wazazi, na upungufu wa walimu waliosomea Elimu maalum katika Vitengo na Shule jumuishi.
Baada ya kuwasilishwa kwa changamoto zinazoikabili sekta ya Elimu katika Mkutano wa wadau wa Elimu, Mwenyekiti aliruhusu mjadala wa wazi kwa wadau wa Elimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo ili kuweza kuinua ufaulu wa wanafunzi.
Wajumbe wa Mkutano huo walichangia hoja mbalimbali kama suluhisho na mwarobaini wa kuinua kiwango cha Elimu sanjari na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za Msingi na Sekondari kama madarasa,maabara,nyumba za walimu,upatikanaji wa walimu wa sayansi,madawati na motisha kwa walimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu Ndugu Emmanuel Johnson aliwapongeza wadau wa Elimu kwa kuzichambua changamoto zinazoikabili sekta ya Elimu na kuwataka wadau wa Elimu kufanya kazi bega kwa bega na Halmashauri na wadau mbalimbali wa Elimu katika kutatua kero zinazoweza kuipandisha taaluma na hatimaye kutoka hatua tuliyonayo kwenda hatua nyingine
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya Ndg. Shija Ntelezu alitoa maoni yake kwa kuwataka wazazi kama wadau wakubwa wa kuinua ufaulu wa mtoto kutimiza wajibu wao na siyo kuwaachia walimu pekee katika suala la kumlea mtoto.
Wazazi tutimize wajibu wetu katika kuinua kiwango cha Elimu kwa watoto wetu pasipo kuwaachia walimu pekee,mwalimu ana nafasi yake katika kumlea mtoto na mzazi pia ana wajibu wake, tukitekeleza wajibu wetu kiwango cha Elimu kitapanda . Ntelezu alisema
Aidha Mwenyekiti wa Mkutao huo Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude aligawa Tuzo kwa Shule zilizofanya Vizuri Katika Mitihani kwa mwaka 2023
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa