Wilaya ya Kishapu imeadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani ambapo mwito umetolewa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kujua iwapo wameathirika na Virusi Vya Ukimwi (VVU huku akikemea unyanyapaa kwa waathirika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Afisa Tawala, Juvenali Byekwasho kijiji cha Bubinza kata ya Mwamashele aliwataka viongozi kuwahamasisha wananchi kupima na afya zao.
Katika maadhimisho yaliyoenda sambamba na zoezi la upimaji VVU ambapo wananchi 143 walipima huku wawili wakikutwa na maambukizi, Byekwasho alisisitiza viongozi wahakikishe wanaendeleza mkakati wa Serikali wa kuhakikisha unyanyapaa unakomeshwa katika jamii.
Alisema maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanaikumbusha jamii kuchukua tahadhari na vichocheo vya VVU na kuwa nguvu kazi inapungua panapokuwa na jamii ya waathirika.
Alitoa rai kwa jamii kuacha mila na desturi zinazochangia maambukizi zikiwemo ndoa za mitala na za umri mdogo, kiwango kidogo cha tohara kwa wanaume na kiwango kikubwa cha maradhi ya ngono.
Aidha, aliishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na Shirika la TCRS kwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ukimwi kupitia shughuli mbalimbali.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Mratibu wa Shughuli za Kudhibiti Ukimwi Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Abednego Madole alibainisha kushuka kwa kiwango cha maambukizi kuwa kufikia Desemba 2016 ni asilimia 4.6 kutoka asilimia 4.9 mwaka 2015 kwa mujibu wa takwimu za ndani.
Alisema hali hiyo ni kutokana na jitihada zinazofanywa na Halmashauri ikishirikiana na wadau mbalimbali ambapo uelewa wa jamii kuhusu Ukimwi umeongezeka sambamba na uwepo wa huduma za kuzuia maambukizi kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hata hivyo pamoja na hayo alisema zipo changamoto zinazochochea maambukizi zikiwemo mikusanyiko ya watu kama sherehe za asili, magulio, minada sehemu za uchimbaji wa madini.
Alitaka elimu iendelee kutolewa kwa jamii na pia suala la Ukimwi kuwa agenda muhimu katika kila vikao na mikutano jambo ambalo litasaidia kuendelea kuikumbusha jamii kuhusu tatiuzo hili.
Itakumbukwa kuwa maadhimisho haya ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika mkoani Lindi ambapo kaulimbiu ni Changia Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi, Okoa Maisha
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa