Halmashauri ya wilaya ya Kishapu imefanikiwa kutambua, kusajili na kupiga chapa jumla ya ng’ombe 100,000 hadi kufikia Novemba mwaka huu, zoezi linaloendelea hivi sasa.
Afisa Mifugo na Maendeleo ya Mifugo wa halmashauri ya wilaya hiyo, Dk. Alphonce Bagambabyaki alibainisha hayo ambapo alisema zoezi hilo ambalo limeweza kuzifikia kata zote za tarafa ya Kishapu.
Alisema zoezi hilo lililozinduliwa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Mh. Nyabaganga Taraba linafanywa na wataalamu wa mifugo kutoka makao makuu wakishirikiana na wataalamu wa kata mbalimbali.
Alisema wilaya hiyo yenye jumla ya ng’ombe 393,371 inatekeleza zoezi hilo ikiwa ni agizo la Mh. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo linataka mifugo yote nchini kutambuliwa kwa kutumia chapa chini ya sheria ya utambuzi namba 12.
Wakati akizindua zoezi hilo hivi karibuni, Mh. Taraba alibainisha zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa ng’ombe kwa kutumia chapa litapunguza changamoto zinazowakabili wafugaji.
Alibainisha kuwa Kishapu ni miongoni mwa wilaya ambazo baadhi ya wafugaji wake wanakabiliwa na matatizo yakiwemo wizi wa mifugo, migogoro na magonjwa hivyo zoezi hili litasaidia kuyapunguza.
Aidha aliwataka wataalamu wa mifugo na watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo ambalo linatarajiwa kufanyika vijiji vyote vya wilaya hiyo vyenye mifugo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa