Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa ushirikiano na Shirika la Msaada na Mandeleo ya Jamii (REDESO) imepima viwanja 196 kwa ajili ya kutolewa hati za kimila kwa wananchi hadi kufikia Novemba mwaka huu.
Zoezi hilo linaendelea katika vijiji vya Negezi, Shagihilu na Ndoleleji ambapo wananchi wanafikiwa na timu ya wapimaji kutoka Idara ya Ardhi na Mazingira halmashauri hiyo.
Hayo yamebainishwa kwenye mdahalo maalumu wa umiliki ardhi na matumizi bora ya ardhi katika halmashauri hiyo zoezi linalofanyika kuwafikia wananchi wa vijiji vya Shagihilu, Ndoleleji na Negezi.
Akizungumza katika mdahalo huo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mh. Boniphace Butondo alisema kuwa hati za kumiliki ardhi zina faida kubwa ikiwemo kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Alisema mwananchi anapokuwa na hati anakuwa katika nafasi nzuri ya kupata mkopo ambao anaweza kuutumia katika kununulia pembejeo za kilimo kama trekta.
Alisema wananchi wanahitaji ardhi iliyomilikiwa kisheria ambapo wataweza kuitumia katika kilimo hususan cha mkonge kama ambavyo wilaya hiyo inavyokienzi.
Aliipongeza REDESO kwa kuhamasisha na kufadhili zoezi hilo la utoaji hatimiliki za ardhi kwa wananchi wa kipato cha chini na hivyo kuwa na haki ya kumiliki ardhi.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Lagana alisema zipo sheria kandamizi kuhusu umiliki wa ardhi hivyo zoezi hili la uandaaji wa hati litawasaidia wanawake kutoka kwenye unyanyasaji.
Kwa upande wa washiriki wa mdahalo huo walibainisha kuwa zoezi hilo litasaidia kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo yao ikiwemo wajane kunyanyaswa. Walisema wameweza kupata urahisi wa kumiliki ardhi tofauti na ilivyokuwa zamani.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa