Na Ofisi ya Habari,Kishapu
Maafisa Ardhi wa halmashauri za Meatu,Maswa,Shinyanga na Kishapu wamekutana hivi karibuni katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa misingi ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika suala zima la utoaji hati miliki ardhi za kimila kwa mujibu wa sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999.
Katika kikao kazi hicho kilichoitishwa kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la OXFAM na kufunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba,wataalamu wa Ardhi walipeana mbinu mbalimbali za namna ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima maeneo yao na kupatiwa hati miliki za kimila kwa mujibu wa sheria.
Mkuu wa wilaya katika hotuba yake ya ufunguzi alilishukuru shirika la OXFAM kwa kuwawezesha kukutana wataalamu hao kwa halmashauri za mikoa hii miwili na kusema wataalam wa ardhi ndio suluhisho la migogoro ya ardhi nchini kama wataitumia taaluma yao ipasavyo,kwani wananchi wakipata elimu ya umuhimu wa kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria na wakaelezwa faida zake kwa kina hakuna mwananchi atakayesita kumiliki ardhi.
Aidha alizitaka kamati za ardhi za vijiji ziundwe ama zifufuliwe na zianze kufanyakazi zake rasimi kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya vvijiji namba 5 ya mwaka 1999 na kanuni zake sanjari na kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi na kupata hati miliki za kimila.Pia aliwataka maafisa ardhi wawe tayari muda wote katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria za ardhi na michakato ya upatikanaji wa hati miliki za kimila bila kuficha.
Naye meneja wa OXFAM kanda ya ziwa ambaye ndio mfadhili katika mradi wa kuhamasisha wananchi kumiliki ardhi na kupata hati za kimila hususan wanawake Bwana Boniventure Kagayo alisema kuwamilikisha akina mama ardhi ni jambo la muhimu kwani ndiyo watumiaji wakubwa wa rasilimali hii na akatoa uzoefu kutoka halmashauri ya Maswa na Shinyanga wananchi wamepewa elimu ya umiliki wa ardhi wameelewa na wamekuwa na mwitikio chanya kuhusu kuwamilikisha wanawake,pia kuwamilikisha wanawake ni suala jema kwani hundoa migogoro ya ardhi katika familia na koo kwani ikitokea mmoja wa wenza amefariki dunia umiliki hubaki ndani ya familia kama kawaida.Aliipongeza halmashauri ya Shinyanga kuweza kupima maeneo ya wananchi na kutoa hati za kimila 286,kati ya hati hizo 50 ni za wanawake,234 ni za wanaume na 1 ni ya umilki wa pamoja.
Katika mjadala huo maafisa ardhi walitoa uzoefu wao katika shughuli zao za kila siku sanjari na kubainisha changamoto zinazowakabili katika utendaji naye Afisa mipango miji wa halmashauri ya Shinyanga Bi Deliqueen Lyimo alisema vijiji vingi havina mipango ya matumizi bora ya ardhi na ukosefu wa masijala za ardhi,hivyo ili zoezi la umilikaji ardhi liende vizuri sharti serikali za vijiji zitekeleze masharti hayo.Pia aliongezea kwa kusema wananchi hawana ufahamu wa sheria za ardhi umilki wa ardhi na gharama za maandalizi ya hati kuwa kubwa.
Katika kikao hicho walihitimisha kwa kuahidi kuyatumia mazuri yote waliyoyapata kwa ufanisi wa halmashauri na serikali kwa ujumla ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua ama kutoweka kabisa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa