Vifo vya wanawake wajawazito wakati wa kujifungua, utapia mlo na udumavu wa afya kwa watoto chini ya umri vhini ya miaka mitano vimeanza kupungua katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Hali hio imesababishwa na jitihada za wadau wa afya kushirikiana na serikali kufikisha elimu ya matumizi sahihi ya makundi matano ya chakula yenye virutubisho muhimu pamoja na madini chuma.
Kauli hio imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Dkt. Shani Josephat Mdamu wakati akikagua mradi maalumu wa mapishi lishe wenye lengo la kuwaokoa watoto wenye utapia mlo na udumavu wa afya katika Kijiji cha Ushiteleja kata ya Mondo Wilayani kishapu ikiwa ni sehemu ya mradi wa Enrich unaotekelezwa na shirika ka World Vision.
“Lakini tunaona kabisa kwenye jamii kuna mabadiliko makubwa kwa maana ya kwamba wanatumia vyakula ambavyo vinapatikana kwenye jamii yao kwa ajili ya kuboresha afya ya mama mjamzito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano” alisema Dkt. Shani.
Nao baadhi ya wanawake waliowezeshwa elimu ya mapishi lishe wamezungumzia hali ya udumavu wa afya na utapia mlo ulivyokuwa changamoto katika familia zao kabla ya kupata elimu ya lishe.
“Hali ya mwanangu ilikuwa mbaya ila sasa yuko vizuri, zamani mara kwa mara nilikuwa namleta mtoto zahanati kwa ajili ya kuharisha na kutapika, lakini baada ya kupata elimu ya darasa la mapishi anaendelea vizuri wala haarishi na kutapika kama mwanzo” alisema mzazi.
Naye Dkt. Frank Mtimbwa ambaye ni Afisa mradi kutoka shirika la World Vision ameahinisha mafanikio yaliyopatikana katika mradi huo.
“Ukiangalia takwimu za mkoa wa Shinyanga utaona vifo vya akina mama na watoto wachanga vimepungua kwa sababu wanapata lishe bora na wanalima mazao yenye virutubisho kwa sababu moja ya lengo la mradi ni kuhamasisha kilimo cha mazao yenye virutubisho” ameongeza Dkt Mtimbwa.
Katika wilaya ya Kishapu takwimu zilikuwa zinaonyesha kwa akina mama walio katika umri wa kuzaa wingi wa damu ulikuwa ni changamoto kwa sababu kati ya akina mama 100, akina mama 59 walikuwa na changamoto ya upungufu wa damu. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya tumefanikiwa kupunguza hii hali kwa asilimia kubwa sana, Hivyo wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia makundi yote matano ya chakula kwa usahihi ili kulinda na kuboresha afya zao..
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa