Mafunzo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu yamefanyika leo Januari 18, 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu yaliyolenga kuwajengea uwezo juu ya masuala yanayohusu shughuli za ujasiriamali zikiwemo kilimo, ufugaji, unenepeshaji wa ng’ombe, ushonaji na uchinjaji wa nyama.
Sambamba na mafunzo hayo wajasiriamali hao wamapata mkopo bila riba kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kishapu ambapo kiasi cha shilingi milioni 34,460,122 zimetolewa kwa ajili ya kunufaisha vikundi kutoka katika kata za Somagedi, Bunambiyu, Ngofila, Lagana, Songwa, Bubiki, Mwamashele, Kishapu, Ukenyenge, Masanga na Mwadui Luhumbo.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ndugu Emmanuel Johnson amewataka wajasiriamali hao kufanya ujasiriamali wenye tija na manufaa huku akisisitiza kurejesha fedha walizokopeshwa kwa wakati ili zinufaishe na wengine.
“Kwa kuwa serikali inawajali, imewaamini kwa kuwakopesha bila riba ili mfanye kilimo na ufugaji wenye tija. Hivyo fedha hizi mkazitumie vizuri na kuzirejesha kwa wakati ili na wengine wapate nafasi ya kunufaika na mkopo huu kama ilivyokuwa kwenu ninyi” amesema Johnson.
Mafunzo hayo yaliyohusisha vikundi 7 vya wanawake, vikundi 4 vya vijana na vikundi 3 vya watu wenye ulemavu vilinufaika na mafunzo hayo ambapo walipewa mbinu mbalimbali za ujasiriamali akiwa ni jinsi ya kunufaika kupitia vikundi vidogo vidogo vya ujasiriamali.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, Joseph Swalala amewataka kuzalisha bidhaa bora zenye thamani ili kuwa na ushindani sokoni, aidha kuichukulia shughuli ya ujasiriamali kama ni ajira kwao hivyo waongeze thamani kwa kile wanachokizalisha.
Naye John Rugembe Sheka ambaye ni mnufaika wa mafunzo haya na mwanakikundi kutoka Kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge anayejishughulisha na shughuli za kilimo cha mbogamboga na viazi lishe ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu kwa kuwajali kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali na mkopo usiokuwa na riba pia ametoa wito kwa wanavikundi wenzake kutumia fedha hizi vizuri ili kujiletea maemdeleo na kuwainua kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa