Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa amesema kuwa Serikali ina mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba kutoka tani 121,000 mwaka 2016/2018 hadi kufikia milioni 1 mwaka 2020.
Mhe. Mkapa amesema hayo leo Agosti 8, 2018 wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) kitaifa yaliyofanyika viwanja vya Nyakabindi Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.
Alisema kuwa mkakati wa Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya uzalishaji wa malighafi za kilimo, uvuvi, mifugo na maliasili na masoko ya uhakika wa bidhaa hizo.
Mkapa ambaye alimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli aliitaka Wizara ya Kilimo kutenga maeneo ya kuzalisha mbegu bora za zao hilo pamoja na kuhamasisha kampuni kuzalisha mbegu bora kwa ajili ya wakulima.
"Ili Taifa lipige hatua lazima tuwabadilishe watu kifikra wafanye kazi kwa bidii katika kuleta maendeleo na tutoe elimu kwa wakulima pamoja na kuwapatia vitendea kazi ili kufanikisha lengo la kukuza uchumi wa viwanda", alisema Mkapa.
Aidha, kutokana na umuhimu huo alitaka maonesho ya Nanenane yalenge kuonesha teknolojia za kisasa kwa wakulima ili waweze kufanya kilimo chenye tija na hivyo kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.
Mhe. Mkapa aliongeza kuwa maendeleo hutegemea watu wanavyofanya kazi na hivyo alitoa mwito kwa kila mwanachi kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu ya kazi.
Kwa upande mwingine alisema kuwa Serikali inawakumbusha wananchi wote kuhifadhi akiba ya chakula wakati wanapouza mazao na hivyo kuhakikishia usalama wa chakula kwenye kaya zao.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa