Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga amewataka wakuu wa shule wilayani hapa kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri katika ufundishaji.
Magoiga ametoa agizo hilo wakati akikabidhi vifaa vya maabara za masomo ya sayansi kwa vitendo ambazo ni stuli 135 kwa ajili ya shule tano ikiwa ni mkakati wa kuboresha elimu.
Akizungumza na walimu wakati akikabidhi msaada huo wenye thamani ya sh. Milioni 6.75 uliofadhiliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R), Magoiga alisema nchi ya viwanda inatokana na masomo ya sayansi.
Alisema kuwa kwa kuboresha sekta ya elimu na afya ambayo ndiyo kipaumbele chake kutakuwa na wasomi ambao ndio chachu ya maendeleo ya na hivyo aliwasisitiza walimu wawape wanafuzni wao mazoezi waelewe vizuri somo hilo.
Aidha, alitoa agizo kwa kwa walimu kuhakikisha wanafunzi wa shule wilayani hapa kuhakikisha wanatumia vizuri stuli hizo ambazo ni muhimu kwa masomo ya sayansi kwa vitendo.
“Niwaombe wakuu wa shule mzifikishe stuli hizi sehemu zinazotakiwa na zitumike kwa malengo yalikusudiwa na nitegemee kila mmoja azitunze zitumike vizuri ili watoto wetu wajifunze vizuri kwa vitendo.
“Nataka mzitumie vizuri stuli hizi na muoneshe tofauti na ilivyokuwa zamani nataka matokeo mazuri, ikifika 2018 nisikie shule zote zimefanya vizuri katika mitihani yenu na kila mwalimu awe na mkakati wa kufaulisha wanafunzi,” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Paul Kasanda alisema huo ni mmoja wa miradi mitatu kwa shule za wilaya hiyo ikiwa ni katika uboreshaji wa sekta ya elimu.
Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mangu iliyopo kata ya Shagihilu, vyoo shule za sekondari Bunambiyu na Ukenyenge ambavyo viko katika hatua nzuri.
Kasanda alisema kuwa kutokana na misaada hiyo inayotolewa kutoka Serikali kuu, sekta ya elimu katika halmashauri hiyo itasonga mbele na hivyo ufaulu kwa wanafunzi utapanda.
Kwa upande wake mmoja wa wakuu wa shule zilizopata msaada huo, Mwalimu Hosea Somi aliishukuru Serikali kwa msaada huo mkubwa wa vifaa kwa ajili ya maabara za sayansi.
Mwalimu Somi ambaye Mkuu wa shule ya sekondari Kishapu alisema anaamini shule zitafanya vizuri katika matokeo ya mitihani yao kwa kuwa vifaa vya maabara ni muhimu katika sekta hiyo nyeti.
Shule zilizopata msaada huo wa stuli ni pamoja na Ukenyenge iliyopo kata ya Ukenyenge, Kishapu iliyopo kata ya Kishapu, Mangu katika kata ya Shagihilu, Mwigumbi kutoka kata ya Mondo na Mwamadulu kata ya Lagana.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa