Serikali imewahakikishia wananchi wilayani Kishapu kuwa itaendelea kuwapatia huduma ya maji safi na salama huku ikiwataka kutunza vyanzo vya maji na miundombinu ya maji ili miradi iwe endelevu ili kumtua mama ndoo kichwani kwa kumpunguzia umbali wa kufuata huduma ya maji.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Aprili 22,2022 na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mhe. Jasinta Mboneko ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wadau wa Maji wilaya ya Kishapu ulioandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Kishapu ukiongozwa na Kauli mbiu ya ‘Changia huduma ya maji kwa huduma endelevu;RUWASA Maji bombani’.
Mboneko amesema serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji pamoja na kuleta fedha kwa ajili ya miradi ya maji ili kumtua mama ndoo kichwani.
“Kwa kutambua umuhimu wa maji serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji,tunataka kila kata ipate huduma ya maji safi na salama ili kumtua ndoo kichwani mwanamke kwa kumsogezea karibu huduma ya maji. Wajibu wa wananchi ni kushirikiana na serikali katika kutekeleza miradi pamoja na kulinda vyanzo vya maji pamoja na miundombinu ya maji”,amesema Mboneko.
“Niwakumbushe pia RUWASA mnapotekeleza miradi ya maji hakikisheni mnatambulisha miradi kwa wananchi ili watoe ushirikiano katika miradi hiyo. Ni lazima wananchi wafahamu taratibu na mipango yote ya miradi ili kuhakikisha miradi inatekelezeka”,ameongeza Mboneko.
Mboneko ametumia fursa hiyo kuipongeza RUWASA kwa kazi nzuri inazofanya katika kufuatilia na kutekeleza miradi ya maji huku akiwataka kuongeza kasi ya kutekeleza miradi na kubuni miradi mipya ya maji ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 asilimia 85 ya wananchi wilayani humo wawe wanapata huduma ya maji safi na salama kutoka asilimia 56 iliyopo sasa.
Aidha ameiomba RUWASA kuwaunganishi huduma ya maji wananchi katika maeneo ambayo mabomba ya maji yanapita kwani lengo la serikali ni kuhakikisha tarafa zote zinapata huduma ya maji safi na salama.
Mkuu huyo wa wilaya amewakumbusha watumiaji wa huduma ya maji kulipia Ankara za maji kwa wakati na kulinda miundombinu ya maji huku akiitaka RUWASA kuzikatia huduma ya maji taasisi ambazo hazilipi bili za maji.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Dickson Kamazima amesema lengo la Mkutano huo mkuu ni kukutana na wadau wa maji kwa ajili ya kujadili, kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo katika namna bora ya utoaji huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema RUWASA Kishapu inayo mikakati ya muda mrefu na mfupi katika kutekeleza miradi ya maji huku akieleza changamoto kubwa waliyonayo hivi sasa ni wananchi kuharibu miundombinu ya maji kwa kukata mabomba ya maji na kusababisha huduma ya maji isipatikane kama ilivyokusudiwa.
Mhandisi Kamazima amesema RUWASA Kishapu inaendelea kushirikiana na wadau wa maji kwa kupeleka huduma ya maji huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji kwani baadhi yao wamekuwa wakiiharibu kwa maksudi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Ndg Emmanuel Johnson amesema wajibu wa serikali ni kutoa huduma kwa wananchi hivyo kuitaka jamii kuwafichua watu wanaoharibu miundombinu ya maji ili huduma ya maji iendelee kuwepo kila wakati.
Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Ndg, Shadrack Kengese amesema serikali itahakikisha inaendelea kuleta miradi ya maji na inakuwa salama na endelevu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Hata hivyo , Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Anderson Mandia ambaye pia ni Diwani wa kata ya Ukenyenge ameshauri kuwekwa kwa Luku za malipo ya kabla ‘Pre Paid’ kwa watumiaji wa maji ambao ni wadaiwa sugu zikiwemo taasisi.
Pia ameshauri kuwepo ushirikiano wa dhati baina ya viongozi wa serikali za vijiji na Vyombo wa watoa huduma ya maji ngazi ya jamii ili kuondoa malalamiko yaliyopo kumewakuwa na ushirikiano mdogo hali inayokwamisha utoaji huduma za maji.
Diwani wa Viti Maalum Mhe. Hellena Balaza ameishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka huduma ya maji kwa wananchi na kuomba wananchi wa maeneo ambapo mabomba ya maji yanapita waunganishiwe huduma ya maji.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa