Serikali kupitia Wizara ya Afya imezindua kampeni ya chanjo ya surua na polio ya sindano kuanzia tarehe 17/10/2019 hadi tarehe 22/10/2019. Lengo kubwa la kampeni hii ni kutokomeza kabisa ugonjwa huu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Kiwilaya kampeni hii ya chanjo imezinduliwa katka zahanati ya Mhunze Bakwata iliyopo Mhunze Kishapu ambapo Kauli mbiu ya kampeni hii ikiwa ni “CHANJO NI KINGA, KWA PAMOJA TUWAKINGE”.
Kwa mujibu wa takwimu, kampeni ya chanjo ya surua na polio mwaka huu kwa wilaya ya Kishapu ililenga jumla ya watoto wapatao 77,857 ambapo walengwa wa surua ni jumla ya watoto 52,065 ambao ni kuanzia umri wa miezi 9 hadi miezi 59 (miaka minne na miezi 11) na polio ya sindano walengwa ni jumla ya watoto 25,792 ambao umri ni kuanzia miezi 18 hadi miezi 42 (mwaka 1 na miezi 3 na nusu).
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya surua na polio Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mh. Nyabaganga Daudi Taraba katika hotuba yake amesema kuwa kampeni hii inahusisha watoto wote chini ya miaka miatano pia amesisitiza kuwa wazazi wapeleke watoto wao kwenye vituo vya afya kupata chanjo za surua na polio.
Aidha mganga mkuu wa hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete, Dr. Josephat Shayo amefafamua kuwa, “kama kuna mtoto wa miezi 9 na ameshapata chanjo mwezi uliopita anatakiwa kupata chanjo tena kwenye kampeni hii”.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya ‘morbillivurus paramyxvirus’vinavyoenea kwa haraka. Ugonjwa huu huenezwa kwa watu wa rika zote lakini zaidi kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya hewa kupitia kukohoa ama kupiga chafya kwenye mkusanyiko na dalili zake ni pamoja na vipele vidogo vidogo kwenye ngozi hasa uso nyuma ya masikio na hatimaye kusambaa mwili mzima, homa kali sana kwa siku za mwanzo, macho kuwa mekundu na kutoa majimaji, uchovu wa mwili, vidonda kooni, uvimbe kwenye matezi pamoja na mafua.
Kampeni hio inayofanyika kila baada ya miaka mitano, imelenga kupunguza Kwa kiasi kikubwa kama sio kutokomeza kabisa ugonjwa wa surua na polio ambapo magonjwa haya yanapopuuzwa husababisha ulemevu wa kudumu na hata vifo kwa waathirika. Ikumbukwe kinga ni bora kuliko tiba.
Na catherine J. Ngowi
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa