Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeanza kwa kasi ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji ambao ni mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 1.16.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Stephen Magoiga amebainisha kuwa mradi huo ulianza mwishoni mwa Oktoba mwaka huu baada ya taratibu za manunuzi ya bomba kukamilika ambapo hadi sasa umefikia asilimia 80.
Kazi zilizofanyika na kukamilika ni uchimbaji mtaro wa kulaza bomba umbali wa mita 23,256 ambalo lina kipenyo cha milimita 315 na urefu wa mita 23,256 pamoja na kuunganisha viungio mbalimbali vya bomba na ‘valve’ za kuondolea hewa.
Magoiga alisema kuwa hadi sasa takriban sh. milioni 820 kimetumika kununua mabomba, viungio, dira za maji 1,500 pamoja na shughuli mbalimbali za mradi huo.
Bomba hilo limepitia katika vijiji 16 ambavyo kwa sasa havina huduma ya maji na yanaweza kuhudumia zaidi ya watu 45,000 hivyo Halmashauri inafanya jitihada za kutafuta fedha za kuyasambaza.
Mradi huu ni mwendelezo wa upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika Mji wa Kishapu kupitia Maganzo na Mgodi wa Almasi wa Mwadui.
Itakumbukwa ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji ulihusisha ulazaji wa bomba la maji lenye urefu wa kilomita 70.2 kutoka Old Shinynga na ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji lenye mita za ujazo 1,200 mjini Kishapu.
Halmashauri hiyo iko katika mikakati ya kuiomba Serikali Kuu kuisaidia fedha za kuzambaza maji hayo katika Mji wa Kishapu na vijiji vingine pamoja na kufanya usanifu na kujenga miundombinu ya majitaka.
Aidha inaendeleza utafiti wa vyanzo vingine zaidi vya maji na kuyatumia ya ziwa hilo kuyasambaza vijiji vilivyopo jirani na bomba kuu. Pia kuelimisha jamii juu ya uchangiaji wa gharama za ujenzi, uendeshaji na ukarabati wa miundo mbinu ya maji.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa