Mtama ni mojawapo ya mazao yanayostahimili ukame hapa nchini ambalo limekuwa ni mkombozi wa chakula kwa jamii kubwa ya Kitanzania na hata nje ya mipaka ya nchi yetu ukiacha mahindi na mazao mengine.
Mtama ukisagwa unaweza kutumika kwa kupata unga ili kutumika kwa ajili ya kupikia chakula aina ya ugali, uji, kutengenezea vitafunwa, vinywaji na majani yake baada ya kuvunwa hutumiwa na wafugaji kulishia mifugo.
Kutokana na kustahimili ukame zao hilo limegeuka lulu katika maeneo mbalimbali hapa nchini na miongoni mwake ni Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inayopatikana Mkoa wa Shinyanga.
Kwa bahati mbaya wilaya hiyo imekuwa haipati mvua za kutosha katika baadhi ya vipindi yote hiyo ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia, hali inayosababisha baadhi ya mazao kutofanya vizuri.
Kutokana na hali hiyo wakulima wengi ‘wameshtuka’ na kuanza kulima mazao yanayostahimili hali hiyo hususan mkonge kama zao la biashara na mazao mengine kwa ajili ya chakula likiwemo mtama na uwele.
Yote hiyo ni kutokana na elimu na hamasa kubwa kutoka kwa viongozi wilayani humo pamoja na wataalamu kutoka Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wakiongozwa na mkuu wake, George Kessy wanayotoa kwa wananchi hususan wakulima.
Mwandishi wa makala haya ametembelea baadhi ya mashamba ya wakulima katika kata za Mwaweja, Uchunga na Lagana wilayani humo na kujionea namna zao hilo linavyofanya vizuri pamoja na kutokuwepo kwa mvua za kutosha.
Akiwa katika ziara hiyo alipata wasaa wa kujionea shamba la familia ya Nkinga na kufanya mazungumzo na wakulima Maria Nkinga wa Kata ya Mwaweja pamoja na James Nkinga, ambalo lina ukubwa wa ekari 40 zikiwa zimelimwa zao la mtama.
Ni dhahiri kuwa wananchi wengi akiwemo mkulima Nkinga wamehamasika kulima mtama badala ya mahindi ambayo hayastahimili ukame kwani ukifuatilia katika mashamba mengi mahindi yamekufa kwa ukame.
Akizungumza na makala haya anawashauri wananchi kulima mtama na kuachana na kuachana na kasumba ya kuchagua chakula na kulima mazao kama mahindi ambayo badala ya kustawi yamekufa.
Anaipongeza Idara ya Kilimo kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya namna ya kutekeleza sera ya kilimo kwanza ambayo ndiyo mkombozi wa wananchi hasa wa maeneo ya vijijini.
”Kwa kweli mtama ndiyo mkombozi wangu kwenye kilimo kwani umenitoa na kama unavyoshuhudia hapa umestawi nasubiri tu kuvuna. Kama una shamba la ekari kumi basi nane lima mtama na mbili zilizobaki basi lima hayo mahindi.
”Mi nawashauri wanawake wenzangu tuwe mstari wa mbele katika kulima zao hili la mtama na kama tukifanya hivyo tutaweza kuepukana na kuombaomba chakula,” anasema Nkinga.
Pamoja na mambo mengine mkulima huyo anatoa kilio chake kwa Serikali akiiomba iwapelekee wakulima mbegu ambazo zinastawi kwa haraka badala ya zile zinazochukua muda mrefu kukua na kutoka mazao.
Anasema kuwa wao kama wakulima wanalima mtama pamoja na kuonesha tayari kuchanua lakini kitaalamu unakuwa bado haujakomaa tayari kwa kuvunwa hivyo ni muhimu kubadilisha mbegu na kupata zile fupi.
Kwa upande wake James Nkinga anasema walipata hamasa ya kulima mtama baada ya kubaini kuwa ni zao linaloweza kuwa mkombozi wao katika chakula na biashara ambapo anatarajia kupata magunia mengi nkwa ajili ya kuuza na chakula.
Nini changamoto kwa wakulima wa mtama?
Chochote kizuri hakikosi changamoto na vivyo hivyo kwa wakulima wa mtama ambapo mkulima Nkinga anazibainisha kuwa ni uharibifu unaofanywa na ndege aina ya kwelea, njiwa pori na wadudu fangasi ambao hushambulia mtama.
“Wadudu fangasi wanashambulia sana mtama na kama ukishambuliwa mkulima hawezi kuvuna chochote matokeo yake anapata hasara kubwa kwa vile ametumia gharama kuandaa shamba,” anasema.
Mbegu za aina hii zina punje za kahawia ambazo huweza kustawi kwenye eneo lenye mvua za wastani ambapo hukomaa katika kipindi cha takriban miezi mitatu pamoja na kuzalisha mtama mwingi.
Mbali ya kukabiliana na kwelea pia zinaweza kukabiliana na magonjwa ya zao la matama yakiwemo milia na madoa yenye rangi ya kahawia yanayotokea kwenye majani yake pindi mtama unapostawi.
Nkinga anaongeza kuwa pia mbegu hizo zina uwezo wa kujilinda zenyewe dhidi ya ndege waharibifu kwa kuwa inanesa na kumdondosha ndege chini endapo atataka kuushambulia mtama unaokuwa umestawi tayari.
Paia anataja mbegu nyingine ‘niyonidaga mhela’ ambayo huchipua na kujaa na kuwa hata ukishambuliwa ndege hawawezi kuumaliza na pia ni chungu hivyo wanapojaribu kushambulia huacha mara moja.
Nini kauli ya Serikali kuhusu mtama?
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba anawataka wananchi wabadilike na kulima mazao yanayostahimili ukame hususan mtama huku akilinganisha na wanaolima mahindi kuwa hawapati mavuno.
Taraba anasema amekuwa akihamasisha wananchi walime mtama na kwa waliofuata ushauri huo wamenufaika na wameweza kupata mavuno mazuri ukilinganisha na waliokaidi.
Mkuu huyo wa wilaya anatilia mkazo Sheria ndogo ya mwaka 2008 Halmashauri hiyo inayotaka kila kila kaya kulima zao hilo angalau ekari mbili ili kupata chakula cha kutosha.
Anawataka wataalamu wa kilimo kwenye kata mbalimbali kusimamia sheria hiyo na kuwaagiza kuwatembelea wakulima mashambani ili kuwafundisha namna ya matumizi ya mbegu bora kwani wengi wao hupanda bila utaalamu.
Taraba anasema hata hivyo wakulima wengi wilayani humo wameweza kutekeleza sheria ndogo hiyo lakini wamepata changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maarifa ya matumizi ya aina sahihi za mbegu.
Anapiga marufuku wakulima kuuza mtama kwa ajili ya matumizi mengine yakiwemo pombe pasipo kujiwekea akiba na kuonya atakayefanya hivyo atachuliwa hatua kali ikiwemo kupigwa faini.
Kauli ya wataalamu wa kilimo
Ofisa Kilimo katika wilaya hiyo, Sarai Pura anasema kama idara kupitia kwa wataalamu waliopo kwenye kata mbalimbali wilayani humo imekuwa ikitoa msisitizo kwa wananchi kulima mtama.
Anasema japo wapo baadhi ya wananchi wasiopokea ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta hiyo lakini kupitia wenzao waliolima wanaweza kujifunza na kuchukua hatua ya kulima mtama ili kupata mavuno.
Pura anazungumzia ndege kwelea akiwataka wananchi kutoa taarifa mapema kwa mtaalamu wa kilimo ngazi ya kata ambaye huzifikisha kwenye idara kwa ajili ya utaratibu wa kuomba ndege maalumu ya kunyunyizia dawa.
“Tunapopata taarifa kutoka kata wataalamu wa halmashauri kwa kushirikiana na timu ya kuzuia ndege waharibifu ya kanda huenda moja kwa moja kwenye eneo yalipo mazalia ya ndege hao na kuchunguza eneo hilo na ikibainika wapo taarifa inapelekwa kwa wizara husika (Kilimo na Mifugo) na wao wanaleta ndege ya kunyunyuzia,” anasema.
Anaongeza kuwa kwa mwaka huu mara baada ya kupata taarifa za tatizo hilo tayari ndege hiyo imefanya zoezi hilo la kunyunyizia dawa eneo la Mwadui ambalo ndilo hutumiwa zaidi na ndege hao kama makazi.
Kwa upande wa mbegu anasema wataalamu huhamasisha wakulima wazinunue kutoka katika maduka ya pembejeo na kama hakuna maduka watumie mbegu wanazoona zinafaa.
Ofisa kilimo huyo anawaasa wakulima kupeleka mbegu ambazo zina ubora na zisizochanganyika na nyingine ambazo hazina ubora unaotakiwa ili kupunguza manung’uniko kutoka kwa wakulima.
Aidha, Pura anawaonya baadhi ya wasambazaji wa mbegu wasiokuwa waaminifu wenye tabia ya kuchanganya mbegu hali ambayo inawasababishia wakulima hasara kubwa kwao, wilaya na hata taifa
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa