Agosti 20 mwaka huu wananchi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga walipata heshima ya kuupokea mwenge ngazi ya kimkoa ukitokea wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Ukichagizwa na burudani kutoka katika vikundi mbalimbali vya sanaa, mwenge wa uhuru ulipokelewa katika kijiji cha Wishiteleja kata ya Mondo ambako wananchi walikusanyika kwa wingi kwa ajili ya kuulaki.
Baada ya kuwasili katika viwanja vya shule ya msingi Wishiteleja kijijini hapo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alimkabidhi mwenzake wa Shinyanga, Zainab Telack.
Mwenge wa uhuru ambao kauli mbiu ya mwaka huu ‘Elimu ni ufunguo wa maisha; wekeza sasa kwa maendeleo ya taifa letu’ ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba tayari kwa kukimbizwa wilayani humo.
Ujumbe huo unazingatia vipaumbele na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha elimu ikiwa ni sekta muhimu ya kuzalisha maarifa ya kiuchumi yatakayowezesha kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia kwenye viwanda.
Uboreshaji elimu unakwenda sanjari na ukuaji wa elimu ya ufundi kwa kuweka msisitizo mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu na ndio maana miradi mbalimbali ya elimu imezinduliwa na mwenge.
Akiwa katika wilaya hiyo, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru 2018 kitaifa, Charles Kabeho alikagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu.
Mwenge ulikagua jumla ya miradi 10 ambayo imetekelezwa na Halmashauri ya Wilaya, Serikali Kuu na wananchi yenye thamani ya bilioni 2.2 ambapo minne kati yake ni ya sekta ya elimu.
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu sita na vyumba viwili vya madarasa ya shule ya sekondari Maganzo ulioanza rasmi mwaka 2017 ulikaguliwa na kuzinduliwa.
Mradi huu wenye thamani ya sh. Milioni 141 umegharamiwa na Serikali Kuu kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya walimu pamoja na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, nyumba ya walimu wawili na matundu 14 ya vyoo shule ya msingi Wishiteleja ni mradi mwingine uliopitiwa na mwenge wa uhuru.
Mradi huo wenye gharama ya sh. Milioni 66.6 kutoka Serikali kuu huku kukamilika kwake kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, kuboresha maisha ya walimu na usafi wa mazingira shuleni.
Aidha mradi wa utengenezaji wa madawati wenye thamani ya sh. Milioni 289.3 ulizinduliwa ukiwa na lengo la kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kutokana na Mpango wa Elimu bila malipo ulizinduliwa.
Halmashauri inatumia mapato yake ya ndani kununua jumla ya mabomba (square pipes) 7,500 na mbao 8,400 zilinunuliwa kutoka msitu wa Taifa Buhindi uliopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Vifaa hivyo vitaweza kukamilisha utengenezaji wa jumla ya madawati 3,000 kwa ajili ya kusambazwa katika shule za msingi na 2,000 kwa ajili ya shule za sekondari wilayani Kishapu.
Halmashauri iliingia mkataba na mafundi ambao ni kikundi cha Umoja wa Mafundi Kishapu (UMAKI), hivyo imeweza kuongeza ajira na mahusiano mazuri kati ya wananchi na Serikali yao kwa ujumla.
Lengo la mradi huo ni kuondoa changamoto ya upungufu wa madawati shuleni ambao umesababishwa na mwitiko mkubwa wa wazazi kuandisha watoto wao kutokana na Mpango wa Elimu bila Malipo.
Hivyo, Kiongozi huyo wa mwenge kitaifa, Kabeho anawasisitiza wazazi kuwaandikisha watoto wao shule ili wapate elimu itakayowasaidia katika mazingira yanayowazunguka.
Anafafanua kuwa wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwasomesha watoto wao na si kuwapa majukumu ambayo yanawanyima wasaa wa kwenda shule na kupata elimu.
“Ndugu zangu wazazi hivi sasa tunatambua Serikali yetu ya Awamu ya Tano inaendelea na Mpango wa elimu bure, imefuta ada na michango iliyokuwa mzigo kwa wazazi hivyo mtumie fursa hiyo kuwasomesha watoto wenu,” anasistiza.
Anasema Serikali kwa kushirikiana na wananchi imewekeza katika ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, mabweni, nyumba za walimu, mabwalo na vyoo ili elimu itolewe katika mazingira mazuri.
Anabainisha kuwa tangu mwaka 2015 hadi 2018 idadi ya wanafunzi walioanza chekechea imeongezeka kutoka 917,000 hadi milioni 1.1 huku darasa la kwanza wakifikia milioni 1.6 kutoka milioni 1.3 na darasa la kwanza ni asilimia 85.77
Itakumbukwa Serikali inawekeza katika elimu hususan masomo ya sayansi kwa kusambaza vifaa vya maabara katika shule za sekondari 1625 nchini hatua inayosaidia wanafunzi kusoma kwa vitendo.
Hivyo halmashauri zote zinahamasishwa kukamilisha ujenzi wa maabara tatu kwa masomo ya Fizikia, Baiolojia na Kemia katika shule zote kama lilivyo agizo la Serikali.
Wakati akikagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo, Kabeho anaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye ubora na kwa gharama nafuu.
Aidha, anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha kwa ajili ya uimarishaji wa sekta ya elimu sanjari na afya na jamii kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo hususana miradi ya maendeleo.
“Kishapu mna kitu cha kipekee. hapa ninyi katika miradi yenu mlipopewa fedha ndani ya gharama mmebakiza chenji na mnaongeza miradi mingine kwa fedha hizo hizo hivyo mnafanya kitu cha kuigwa,” anasema.
Mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2018 zimebeba Ujumbe kwa mwaka huu zinalenga kuelimisha, kuhimiza, kusisitiza na kufafanua kwa wananchi umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa kuboresha miundombinu.
Pia kuhimiza masomo ya sayansi na dhana ya mpango wa Serikali wa elimu msingi bila malipo ambapo wilaya inaendelea kuwahamasisha wananchi kuwekeza katika elimu kama hatua muhimu ya kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kusaidia Taifa.
Kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 wananchi wameanzisha shule mpya sita za msingi ambazo ni Ndema, Wizunza, Mwakolomwa, Ijimija, Mwamasololo na Muungano na sekondari mbili za Lagana na Mwanima.
Pia meendelea kuboresha miundombinu na mazingira bora ya kutolea elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa shule za msingi jumla ya vyumba vya madarasa 27 vimekamilika na sita vinaendelea kujengwa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa