NIDA MKOA WA SHINYANGA YA ZINDUA ZOEZI UGAWAJI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA KWA WANANCHI
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoa wa Shinyanga, imezindua rasmi zoezi la ugawaji wa Vitambulisho hivyo kwa wananchi. Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 15, 2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, na kuzinduliwa Rasmi na Mkuu wa Mkoa Mhe. Christina Mndeme, na kisha kuwakabidhi Vitambulisho vya Taifa Wakuu wa wilaya ili vikasambazwe kwa wananchi.
Afisa Msajili wa NIDA Mkoa wa Shinyanga Nathanael Njau akizungumza kwenye zoezi hilo la uzinduzi wa ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa, amesema Mamlaka hiyo imeandaa mpango kazi wa ugawaji wa Vitambulisho hivyo kwa Wananchi pamoja na kuendelea kufanya usajili. “Zoezi hili la ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa linaloendelea tunaomba kupata ushirikiano wako Mkuu wa Mkoa na timu yako katika usafiri na ushauri, ili kuhakikisha uhamasishaji wa zoezi hili unafanyika katika ngazi zote ili wananchi waweze kuitikia wito na wachukue Vitambulisho katika maeneo yao,”amesema Njau.
Aidha, amesema katika Mkoa huo wa Shinyanga wameweza kusajili jumla ya wananchi 718,243 kati ya 833,279 ya waliokusudiwa kusajili sawa na asilimia 86 ya usajili. Pia ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia namna ambavyo imeendelea kuipa nguvu Mamlaka hiyo katika kutimiza majukumu yake, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuendelea kushirikiana nao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, ametoa Maagizo kwa Wakuu wa wilaya mkoani humo mara baada ya kuwakabidhi Vitambulisho hivyo, kwamba wavisimamie na kuwafikia walengwa. Amewataka pia wananchi ambao bado hawajajisajili ili kupata Vitambulisho vya Taifa, kwamba wakajisajili sababu Vitambulisho hivyo ni haki ya kila Mtanzania.
“Tunataka kila Mtu awe na Kitambulisho cha Taifa badala ya kuwa na Namba ya NIDA, nendeni Mkajisajili na Vitambulisho hivi vitawafikia popote mlipo Mheshimiwa Rais hataki wananchi wake wapate usumbufu bali mtaletewa kwenye maeneo yenu,”amesema Mndeme.
Aidha, amewataka pia wananchi wale ambao wamshapoteza Vitambulisho vyao, kwamba wafikie kwenye Ofisi za Msajili ili wapate Vitambulisho vingine.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa