Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ametumia Siku ya Mazingira Duniani kuwaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari zinazotokana na vitendo vya ukataji miti.
Ametoa agizo hilo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba leo wakati wa kilele cha siku hoyo kilichofanyika kimkoa kata ya Mwamashele wilayani hapa.
Alisema kuwa wananchi wengi hawaelewi kuwa tunapokata miti kwa wingi tunatishia uhai wetu na wa wanyama hali inayotokana na ukosefu wa mvua na hivyo kusababisha ukame.
Telack alisema kuwa misitu ndiyo mhimili mkubwa wa kulinda mazingira yetu na kutupatia nishati, dawa za asili, vifaa vya ujenzi pamoja na kuboresha hali ya hewa.
“Pamoja na muhimu wa misitu kwa binadamu na mazingira imekumbwa na uharibifu mkubwa katika mkoa wetu wa Shinyanga kwa matumizi mbalimbali yakiwemo ya uchomaji mkaa,” alisema.
Aliongeza kuwa uchomaji wa mkaa katika maeneo mengi kama vile Nyasamba umekuwa kama shughuli ya kujipatia kipato na hivyo kutishia kutoweka kwa misitu.
Aliwataka wadau kutumia nishati mbadala kama vile vinyeshi vya wanyama na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi hayo kwani matumizi ya mkaa ni adui wa mazingira.
Mkuu huyo wa mkoa alionya kuwa uchomaji mkaa na utumiaji wake huongeza hewa ya ukaa na kusababisha mabadiliko ya tabia ya nchi na hatimaye kuleta ukame.
“Hivyo ni vema wananchi tubadilike na tuachane na matumizi ya rasilimali zetu kuwa endelevu kwa kupanda miti zaidi ili tuhifadhi ardhi, vyanzo vya maji na kuboresha hali ya hewa,” alisema.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Boniface Butondo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga, wakurugenzi wa halmashauri za Ushetu, Msalala, Shinyanga na Kahama.
Sherehe hizo ambazo kitaifa zilifanyika jana mkoani Mara zinachagizwa na kaulimbiu ya Hifadhi ya Mazingira ni muhimili kwa Tanzania ya Viwanda.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa