Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu chini ya ufadhili wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Msaada na Mandeleo ya Jamii (REDESO) imetoa vifaa kwa ajili ya mradi wa bwawa la samaki kwa kikundi.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 4.3 vimetolewa kwa kikundi hicho kilichopo kijiji cha Lubaga huku halmashauri hiyo ikiahidi kutoa sh. milioni 3 kwa ajili kununua vifaranga vya samaki.
Katika makabidhiano hayo, vifaa mbalimbali vikiwemo pampu ya kuvuta maji kutoka kwenye chanzo, wavu wa kuweka juu ya bwawa kuzuia samaki kudhuriwa, mabomba ya kuvuta maji na karatasi maalumu ya kutandika chini kuzuia maji yasinyonywe na udongo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Kishapu, Dk. Alphonce Bagambabyaki aliishukuru REDESO na kuwataka wanakikundi hicho kuutunza mradi kwani utakuwa na manufaa kwao na kijiji kizima.
Alisema mradi huo pia utatangaza kijiji hicho kwa kuwa na kitoweo cha samaki kitakachokuwa kinapatikana hapo na pia kutoa ajira hususan kwa mamalishe hivyo kujenga uchumi.
“Tumewaletea mradi huu hivyo ni jukumu lenu kuutunza na mnatakiwa muweke uzio kuzuia mifugo isiingie bwawani kunywa maji na kuwadhuru vifaranga wa samaki watakaopandwa,” alisema Dk. Bagambabyaki.
Kwa upande wa Afisa Ugani kutoka REDESO, Erica Karutha alisema lengo la mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Irish Aid ni kuwakwamua kimaisha wanawake na vijana.
Karutha alisema kuwa wanaahidi endapo mradi huo utafanya vizuri wataendelea kuwafadhili na hatimaye uweze kuenea katika maeneo mengine ya wilaya hiyo
Alisema shirika hilo linafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji katika halmashuri hiyo na kuwataka wananchi wengine wajitokeze kuchangamkia fursa za miradi kama hiyo.
Kikundi hicho chenye jumla ya wanachama 15 ambao wamejitolea kuchimba bwawa hilo kwa ajili ya kupandikiza vifaranga vya samaki ambapo wamehukuru kwa msaada huo na kuahidi kuutunza.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa