SERIKALI YAFUNGA MACHIMBO YA ALMASI MWANONGO KWA AJILI YA CORONA.
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu iliyopo mkoani Shinyanga leo tarehe 20 Machi 2020 imefunga machimbo ya Mwanongo yaliyopo katika kata ya Maganzo. Machimbo hayo yalivamiwa na wananchi kinyume cha sheria kwa kuchimba almasi bila kibali maalumu.
Kwa mujibu wa Afisa madini mkoa wa Shinyanga, Injinia Joseph Kumburu amekiri kupokea taarifa ya wachimbaji madini kuvamia eneo la Mzee Majebele Nsonda na kusema kuwa eneo hilo limevamiwa na kuchimbwa madini kinyume na sheria ya madini nchini Tanzania kwani lina leseni kubwa ya ushimbaji madini.
“Maelekezo ya waziri wa Madini tumeyasikia kwenye maeneo ya uchimbaji kuwa tuzingatie kuweka vifaa kingakwa ajili ya COVID-19 sasa katika hili eneo hatuwezi kuweka kwa sababu watu wamevamia bila kufuata taratibu za uchimbaji madini. Vile vile kutokana na uchunguzi tuliofanya na jeshi la polisi na vyombo vingine tuligundua kumekuwa na hali ya utoroshwaji wa madini mkubwa sana kwani madini yaliyochimbwa hapa yalikuwa hayaendi sokoni. Hivyo sisi kama Ofisi ya Madini tulifanya majadilino na Halmashauri ya Wilaya tukachukua hatua ya kusitisha zoezi la kuchamba madini hayo”
Katika machimbo hayo watu zaidi ya mia tatu walikuwa wanajihusisha na shughuli hio hali iliyopelekea kuzua kwa taharuku ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu ugonjwa hatari wa COVID-19 kutokana na mkusanyiko wa watu katika eneo husika.
Kwa mujibu wa Afisa Afya wa wilaya ya Kishapu, Erick Yossam Muhigi alisema mazingira hayo sio rafiki kwa afya za watu kwani kulingana na hali ya hewa ya mvua hakuna choo na mkusanyiko wa watu ni mkubwa sana hivyo inaweza pelekea magonjwa.
“ Tujali afya zetu kwanza kwa kuhakikisha tunafanya kazi kwenye mazingira salama, kutokana na hili gonjwa jipya la CORONA kwa ajili ya tahadhari ya afya tuondoke kwanza kwenye mazingira haya ili kupisha huu ugonjwa na taratibu nyingine za kiserikali kufanywa.Pia kutokana na hali ya hapa hakuna vyoo, hivyo kinga ni bora zaidi kuliko tiba”
Aidha serikali imetoa tamko kwa wamiliki wote wa leseni wanaomiliki maeneo ya uchimbaji kulinda leseni zao. Hata hivyo Mmiliki wa eneo hilo ameandikiwa barua na ofisi ya madini kulipa gharama zote kwa ajili ya uwekezaji uliofanyika katika eneo hilo. Hivyo vyombo vya usalama vitakuwa katika eneo hilo kuhakikisha hakuna shughuli zozote za uchimbaji zinazoendelea.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa