Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Serikali wilayani Kishapu imepiga marufuku wakulima kuchanganya pamba na mazao mengine na badala yake wagawe mashamba yao kwa ajili ya mazao mengine.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Mh.Nyabaganga Taraba wakati wa mikutano ya wakati wa mikutano ya kampeni za kuhamasisha kilimo cha mazao ya biashara na chakula kwenye vijiji vya Bunambiyu na Itongoitale kata ya Bunambiyu .
Mh.Taraba alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za kilimo cha pamba za mwaka 2010 kifungu 11(1) na (2) ni kosa kwa mkulima kuchanganga pamba na mazo mengine na hivyo anaweza kukabiliwa na adhabu ya kulipa faini isiyopungua sh. laki moja au kifungo cha miezi mitatu au vyote.
“Kama tunavyofahamu huu ni msimu wa kilimo na tumeletewa mbegu ya pamba mpya na Serikali inafufua kilimo cha zao la pamba ni wakati sasa kwa wakulima kuanza kufuata kanuni za kilimo bora. Unashauriwa kugawa shamba lako eneo la pamba na eneo la mazao mengine,” alisema.
Aidha Mh. Taraba akiwa ameambatana na timu ya wataalamu wa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama alisisitiza umuhimu wa kufuata kanuni za kilimo.
Mkuu huyo wilaya alisema Kishapu inaongoza kwa kilimo cha pamba na hivyo aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kulima zao hilo kubwa la biashara ili wapate maendeleo na kubadilika kimaisha.
Alisema lengo la kampeni hiyo ni kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu agizo la Serikali la kusimamia kilimo hicho ambapo Kishapu imeagizwa kulima mazao yanayostahimili ukame yakiwemo pamba, alizeti, mtama na uwele.
“Serikali imeagiza kilimo cha pamba kisimamiwe kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maelekezo yanayotolewa na Serikali mara kwa mara ili kuwezesha wananchi na taifa kuingia kwenye uchumi wa kati na wa viwanda,” alisema.
Kishapu ni miongoni mwa wilaya chache zilizoteuliwa kuanza kutumia mbegu mpya na bora ya pamba UKM 08 katika mchakato wa kufuta mbegu ya zamani UK91 ambayo ilishapoteza sifa.
Huu ni mkakati wa Serikali wa kuongeza tija pamba kutoka uzalishaji wa kilo 200 kwa ekari hadi kilo 800 na 1200 kwa ekari na hivyo ni marufuku kwa mkulima aliyelima mbegu ya UKM08 kuchanganya na UK91 vinginevyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Kampeni hii inafanyika katika kata zote za wilaya hiyo na imedumu kwa muda wa wiki tatu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa