Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu umetoa jumla ya shilingi milioni 237.8 kwa kaya maskini 5948 katika kipindi cha mwezi Machi hadi Aprili.
Mratibu wa TASAF, Sospeter Nyamhanga amesema kuwa katika kipindi hiki fedha za walengwa zimeongezeka kutokana na wengi wao kutimiza masharti ya elimu na afya.
Alisema kuwa zoezi hilo linaloendeshwa katika vijiji 78 wilayani humo limepata mafanikio kutokana na walengwa wengi kufanyia kazi elimu wanayopewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha wanazowezeshwa.
Nyamhanga alibainisha kuwa baadhi ya kaya wameanza kubailika kimaisha kwa kutumia fedha hizo kununua mifugo kama mbuzi na kuku na wengine biashara ndogondogo ambazo huwaingizia kipato.
Alisema kuwa baadhi ya walengwa tayari wamebadilisha aina za makazi yao kutoka nyumba za tembe na nyasi na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali inayoleta matumaini katika miradi kama hii.
“Lengo la mpango wa TASAF awamu ya tatu siku zote ni kuziwezesha kaya maskini kujikwamua kimaendeleo na kiuchumi na ndiyo maana tunatoa elimu ya kuwekeza katika shughuli za kilimo, ufugaji au biashara ndogondogo,” alisema.
Aidha, Nyamhanga alibainisha kuwa pamoja mambo mengine pia walengwa wanapopata fedha hizi wanawajibika kuwapeleka watoto wao shule na kliniki kama ambavyo masharti yanavyoelekeza.
Alisisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto wa walengwa kwani wanavyoelimika ndivyo wanaondosha umaskini na kuchangia kujikwamua katika umaskini kwa kaya zao.
TASAF imekuwa ikitoa ruzuku ya msingi kwa kaya zote maskini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine ya utimizaji masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa kwenda shule na vituo vya kutolea huduma za afya.
Kishapu ni miongoni mwa halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba zinazotekeleza Mpango wa TASAF III ili kuongeza kipato na fursa za kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa