Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amezindua rasmi shughuli za uzalishaji kwenye Mgodi wa uchimbaji madini ya Almasi (Williamson Diamond Limited) uliopo Kishapu Mkoani Shinyanga ikiwa ni takribani miezi nane tangu mgodi huo usitishe uzalishaji baada ya kingo za Bwawa la Maji Tope kubomoka.
Novemba 7,2022 Bwawa la tope la mgodini katika mgodi wa Mwadui lilipasuka na kuharibu makazi na mashamba ya wananchi wa vijiji vya Ng'wanholo na Nyenze vilivyopo katika Kata ya Mwadui Luhumbo wilayani Kishapu kwa kufunikwa na tope.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumatatu Julai 17,2023 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme ameupongeza Mgodi huo kwa kuchukua hatua mbalimbali baada ya kingo za Bwawa la Maji Tope kubomoka na kusababisha athari kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi.
Uzinduzi huo umefanyika siku chache baada ya Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko kuagiza mgodi wa Williamson Diamond Limited uanze shughuli za Uzalishaji kuanzia Julai 15 baada ya kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa.
“Nimezindua rasmi uzalishaji katika mgodi huu. Hongereni kwa hatua hii na kazi iendelee. Naomba shughuli za uzalishaji zifanyike kwa kasi(spidi nzuri) kwa viwango vinavyotakiwa ili tuweze kufidia muda tuliokuwa tumesimama, serikali ipate mapato, ajira ziendelee, halmashauri zipate mapato, miradi ya CSR iendelee na watu wote waliokuwa wanatoa huduma hapa mgodini waendelee na kazi”,amesema Mhe. Mndeme.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa