Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Suleiman Nchambi amewataka wananchi kuwa kichocheo cha miradi ya maendeleo katika maeneo yao bila kujali msingi ya tofauti zao.
Nchambi alisema hayo jana wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Mfuko wa Jimbo kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambapo jumla y ash. Milioni 82 zinatarajiwa kutolewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo
Katika kikao hicho kilichohudhuria pia na madiwani, watendaji mbalimbali na viongozi wa dini alisema wananchi wanaoibua miradi ya maendeleo na Serikali kupitia Mfuko wa Jimbo inawapelekea fedha ili zitumike kufanya miradi hiyo.
Alisema viongozi wa ngazi za kata wakiwemo madiwani na watendaji wana nafasi ya kuhamasisha wanancho wao kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutoa elimu kuhusu fedha za mfuko huo.
Mbunge huyo alibainisha kuwa katika mwaka huu fedha zinazotarajiwa kutolewa katika jimbo hilo zitasaidia katika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata mbalimbali.
Nchambi alizihakikishiwa taasisi na wananchi kuwa tayari kuwasaidia katika hatua za kuunganisha umeme lengo likiwa kila mmoja apate huduma hiyo bila kujali tofauti zao mbalimbali.
Kwa mujibu wa mbunge huyo nishati hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na kuzidi kuimarisha uchumi kwenye jimbo na pia halmashauri ya wilaya nzima kwa ujumla wake.
“Tumuunge mkono Rais wetu ana dhamira nzuri na anataka kila mwananchi awe ameunganishwa umeme kwani umeme utahamasisha maendeleo kwenye jimbo letu na kata zake, tunataka jimbo liwe na shapu shapu,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga aliwataka wanakamati hiyo kuwa makini katika kusimamia fedha za Mfuko wa Jimbo.
Magoiga alisema fedha hizo zinapaswa kufanya kazi ya kuleta maendeleo kwa wananchi na kuwa zinapaswa kusimamiwa vizuri ili kuendana na kauli mbiu ya Rais ya hapa kazi tu.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji na wenyeviti wote wa vijiji kufungua akaunti benki ili kuhifadhi fedha za miradi wanazopokea badala ya kuhifadhi kwenye akaunti binafsi.
Mkurugenzi mtendaji aliwataka kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuwa Serikali itawasaidia pale ambapo watakuwa wameibua miradi ikiwemo kuanzisha majengo ya huduma za kijamii.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kwa kutoa mabati 171 kwa ajili ya kuezekea vyumba vya madarasa katika shule za msingi akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga Kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa