Wanawake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi wa majengo ya kituo cha afya cha Songwa yakiwemo chumba cha upasuaji.
Katika maadhimisho hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala Wilaya, Shadrack Kengese walibeba mchanga ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kengese aliikumbusha jamii kuwa na wajibu mkubwa katika kushriki kupiga vita unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa wanawake katika maeneo mbalimbali.
Aliongeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyopo katika jamii yanayomnyima mwanamke haki zake mbalimbali ni mila na deturi zinazowabagua na kuwakandamiza wanawake.
“Mwanamke asipopewa kipaumbele katika suala zima la elimu na hata kunyimwa fursa ya kushirikishwa katika maamuzi au kutokuwa na uwiano katika ugawaji rasilimali anakuwa ananyimwa haki zake.
“Kupitia maadhimisho haya naamini kila mmoja wetu ametambua mchango wa mwanamke katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hivyo natoa rai kila mmoja wetu apinge masuala yanayomkandamiza na kumnyanyasa mwanamke,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa maadhimisho yamelenga kumkumbuka kila mwanamke na kuthamini jitihada zake katika shughuli za maendeleo na kuchukua hatua za kukabiliana changamoto zinazowakumba.
Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila Machi 8 ambapo katika Wilaya ya Kishapu imeadhimishwa kata ya Songwa huku kaulimbiu yake ikiwa ni ‘Kuelekea Uchumi wa Viwanda Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini’.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa