Na Ofisi ya Habari,Kishapu
Umoja wa Wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamesherehekea Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa misaada ya vyakula na vitu mbalimbali kwa wahitaji.
Katika maadhimisho hayo wanawake hao walitoa misaada mbalimbali ambayo jumla ya thamani yake ni sh. 524,000 kwa watu wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali ya mkoani Shinyanga.
Walitembelea na kufariji wagonjwa waliolazwa Hospitali ya Wilaya ya Dk. Jakaya Kikwete, familia ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kituo cha kulelea walemavu cha Buhangija.
Wanawake hao wakiwemo watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo walitembelea wazazi waliojifungua hospitalini hapo na kuwapa misaada mbalimbali ikiwemo sabuni ikiwa ni njia ya kusherekea nao.
Katika ziara hiyo ya wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu waliitembelea familia ya watu wenye ulemavu wa ngozi wilayani hapo na kukabidhi msaada wa vyakula, mafuta na sabuni.
Pia walitumia nafasi hiyo kufika katika kituo cha kulelea watoto hao kilichopo Manispaa ya Shinyanga eneo la Buhangija ambacho hulea watoto walemavu wa ngozi na kutoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula vifaa vya kufanyia usafi na masufuria makubwa sita.
Aidha, wanawake hao waliungana na wenzao kutoka wilaya ya Shinyanga kuadhimisha sherehe hizo wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack katika viwanja vya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Telack aliwataka wanawake kuwa chachu ya mabadiliko kwa kubuni miradi ya maendeleo ili kupata vipato vya familia na kujikwamua kiuchumi.
Alisema wanawake ni msingi wa mabadiliko kiuchumi na kuwa wana nafasi kubwa ya kukuza uchumi huku akiwataka wanaume wawape nafasi na kuachana na mfumo dume ambao ni mwiba kwa maendeleo ya wanawake.
”Wanawake sasa wako mstari wa mbele kuzalisha wanachohitaji, nawapongeza kwa kazi nzuri, navipongeza vikundi vya wajasiriamali na nawaomba tuzalishe kwa viwango bidhaa zenu mpate masoko kutoka nje ya nchi,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande mwingine Telack aliagiza idara za Maendeleo ya Jamii katika halmashauri kuwa na utaratibu wa kuwawezesha wanawake wapate masoko makubwa na watoke walipo wasonge mbele.
Pia alizitaka taasisi za kifedha nchini zisadie wanawake kwa kuwapa elimu ya mikopo na faida zake namna ambavyo wataitumia kuanzisha ujasiriamali lengo likiwa ni kujikwamua kiuchumi.
Aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kupima saratani ya shingo ya kizazi zoezi litakalofanyika Jumamosi Hospitali ya mkoa ikiwa ni mojawapo ya sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo.
Sherehe hizo za Wanawake ambazo kaulimbiu yake ni ‘Tanzania ya Viwanda, Wanawake ni msingi wa mabadiliko kiuchumi’ zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu ,Helen Chacha, Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Agnes Machiya.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa