Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Seleman Jafo, ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi (EBARR) wilayani Kishapu.
Jafo amebainisha hayo leo Mei 6,2023 wakati alipofanya ziara wilayani Kishapu, kutembelea kuona utekelezaji wa miradi hiyo ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema katika ziara yake wilayani Kishapu ya kutembelea miradi hiyo ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, ameridhika nayo baada ya kuona imetekelezwa vizuri, huku akiagiza kwa ile ambayo bado haijakamilika ikamilike haraka kabla ya mwaka wa fedha mwezi Julai iwe tayari na kuanza kutumika.
“Nimeridhika na ziara yangu hapa Kishapu nimeona miradi iko vizuri, na Rais Samia anapoona miradi ambayo anatoa fedha inatekelezwa vizuri anafarijika sana,”anasema Waziri Jafo.
“Naomba wananchi muitumie vyema miradi hii kwa tija, pamoja na kutunza mazingira kwa kupanda miti,”ameongeza.
Aidha, Miradi ambayo Waziri Jafo ameitembea ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mingine kuweka jiwe la msingi na kuzindua ni Mradi wa unenepeshaji Mifugo katika Kijiji cha Muguda, na kuweka jiwe la msingi katika jengo la kusaga mahidi na kukamua Alzeti, Bwawa la Maji Kijiji cha Kiloleli na Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi vikiwamo viatu.
Miradi mingine ambayo inatekelezwa ni ujenzi wa Majosho, Majiko Banifu yatakayosaidia kupunguza matumizi ya kuni, ufugaji wa nyuki, na kilimo zao la Mkonge,
Anesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kutekelezwa miradi hiyo ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, ili wananchi wawe na shughuli mbadala za kufanya ambazo zitawaingizia kipato na kuacha kuharibu mazingira kwa kukata miti hovyo ikiwamo kufanya biashara za kuchoma mikaa.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo, ameziagiza halmashauri zote hapa nchini kutekeleza agizo la upandaji miti Milioni 1.5 kwa kila mwaka, pamoja na kuihamasisha kampeni ya soma na mti ambayo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amesema Serikali ilipeleka kiasi cha fedha Sh.bilioni 1.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi. ambayo inatekelezwa katika Kata mbili ya Lagana na Kiloleli, na imekuwa na tija kwa wananchi katika suala zima la utunzaji wa Mazingira.
Nao baadhi ya wananchi ambao ni wanufaika wa miradi hiyo, wameishukuru Serikali kwamba licha ya kutunza mazingira, pia imekuwa ikiwasaidia kuwaingizia kipato na kuendesha maisha yao.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa