Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni .M. Mhita akizungumza katika kikao maalumu na madiwani wa Wilaya ya Kishapu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni .M. Mhita amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Disemba 18, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, ambapo amekutana na baraza jipya la Madiwani pamoja na wakuu wa divisheni na vitengo vya Halmashauri hiyo.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuzungumza na madiwani 39 wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, kuwapongeza na kuwaambia kuwa wananchi wana imani kubwa juu yao katika kuwasilikiza na kutatua kero zao, huku akiwataka madiwani hao kudumisha ushirikiano na mshikamano kama nguzo ya kufanikisha mipango ya maendeleo. “Udiwani ni dhamana ambayo wananchi wamewapatia kuwa na imani kubwa na ninyi,hivyo mna dhamana kubwa kwao kama wawakilishi wao kuwasikiliza na kuwajibika.” Amesema Mhe. Mhita.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alipokelewa na kukaribishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Ndg. Emmanuel Johnson, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kishapu Mhe. Josephat Limbe.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mhita amewasisitiza madiwani hao kutimiza majukumu yao ipasavyo, sambamba na kuimarisha demokrasia baina yao na wananchi kwa kuitisha mikutano ya hadhara mara kwa mara na wananchi wa kata zao ili kutatua changamoto zinazowakabili. Aidha amesema miradi ya maendeleo izingatie maslahi mapana ya wananchi wa Wilaya ya Kishapu.


Madiwani wa kata mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wakisikiliza kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Disemba 18,2025.
Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita inaendelea kuwalinda viongozi wote, wakiwemo madiwani katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao bila kuathiriwa na nia ovu kutoka kwa baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa ameutaka uongozi wa Halmashauri na menejimenti yake vyanzo vipya vya kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo, kadhalika kubuni mifumo thabiti ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shiyanga Mhe.Peter Masindi akizungumza katika kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Disemba 18, 2025.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri kwa niaba ya madiwani amemshukuru Mkuu wa mkoa kwa maelekezo na ushauri aliowapatia, huku akiahidi kuyafanyia kazi kwa weledi na uadilifu kupitia ilani ya chama ili kuleta matokeo chanya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Josephat Limbe akizungumza katika kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Disemba 18,2025.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kishapu Ndg. Emmanuel Johnson amesema kuwa yeye pamoja na menejimenti yake wataendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuwaletea wananchi huduma bora na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
“Menejimenti kwa ujumla wake tutaendelea kusimamia na kutekeleza maelekezo yote uliyoyatoa, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa thamani ya fedha na kwa maslahi mapana ya wananchi.” Amesema Mkurugenzi

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu akizungumza katika kikao maalumu cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Disemba 18,2025.


Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu pamoja na wawakilishi kutoka taasisi tofauti wakifuatilia kikao kazi cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, kilichofanyika katikaukumbi wa Halmashauri hiyo, Disemba 18, 2025.
Ziara hiyo imeudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kishapu, Katibu Tawala wa Wilaya, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa, wawakilishi kutoka Taasisi tofauti pamoja na wajumbe wa kamati ya usalama wa Mkoa na Wilaya.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa