Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu limepitisha rasmi bajeti ya Shilingi bilioni 1, zilizotolewa na Mgodi wa Almasi Mwadui kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Uamuzi huo umefanyika leo, Juni 13, 2025, katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha matumizi ya fedha hizo.

Afisa Mipango na Mratibu wa CSR katika Halmashauri ya Kishapu, Bw. James Zitto, akiwasilisha bajeti hiyo alisema kuwa fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo katika jamii pamoja na miradi ya kimkakati ya halmashauri.

“Asilimia 40 ya fedha hizi zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka mgodi, na asilimia 60 zitatumika kwa miradi ya kimkakati ya halmashauri,” alisema Zitto.

Baada ya mjadala wa kina kutoka kwa madiwani, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri aliomba baraza liridhie bajeti hiyo ambapo kwa kauli moja, madiwani waliidhinisha rasmi.

Mkurugenzi wa Halmashauri, Bw. Emmanuel Johnson, aliwataka madiwani kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa uadilifu mkubwa na kuonya dhidi ya migogoro ambayo inaweza kuathiri utoaji wa fedha hizo kutoka mgodini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mheshimiwa Peter Masindi, alitoa wito kwa viongozi kutowaingilia wakandarasi wala kuwaomba “kitu kidogo”, akisisitiza kuwa tamaa binafsi zisiharibu sifa ya viongozi wala kusababisha miradi hiyo kufeli.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa