Mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Afisa Elimu Sekondari, David Mashauri akikabidhi vifaa hivyo Januari 27,2025
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa waalimu wenye changamoto ya uoni wanaofundisha katika Shule ya Sekondari Shinyanga, hatua inayolenga kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza ubora wa utoaji elimu.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Afisa Elimu Sekondari, David Mashauri, amewataka walimu waliopokea vifaa hivyo kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili viweze kuleta tija katika kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa elimu jumuishi.
Amesema Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha walimu wote, hususan wenye mahitaji maalum, wanapatiwa mazingira rafiki yatakayowawezesha kutimiza wajibu wao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na laptop, iPad pamoja na kinasa sauti ambavyo vitawasaidia waalimu hao katika maandalizi ya masomo, ufundishaji na utekelezaji wa majukumu mengine ya kitaaluma kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wao, walimu waliopokea vifaa hivyo wameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa msaada huo. Akizungumza kwa niaba yao, Mwl. Josia Nkinga, amesema vifaa hivyo vitawapunguzia utegemezi kwa kiasi kikubwa, hali itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa haraka, ufanisi na uhuru zaidi.

Mwakilishi wa Walimu kutoka Shule ya Sekondari Shinyanga waliopokea vifaa hivyo Mwl. Josia Nkinga akizungumza kwa niaba ya wenzake
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni chachu muhimu katika kukuza elimu jumuishi na kuwapa motisha walimu wenye changamoto ya uoni kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa