Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Josephat Limbe akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani humo cha kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 54.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Februari 12,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga limeidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 54.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kikao kilichofanyika Februari 12, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo. Kati ya fedha hizo, bilioni 2.8 zimetengwa mahsusi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mhe. Josephat Limbe, amewapongeza Waheshimiwa Madiwani kwa kujadili kwa kina randama ya bajeti kuanzia ngazi ya kamati za kudumu hadi baraza la chama (CCM na ACT Wazalendo) hadi kufikia hatua ya kuidhinishwa rasmi. Akisisitiza umuhimu wa usimamizi wa mapato ya ndani, amesema: “Nawasihi madiwani kushiriki kikamilifu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ndani ya kata zenu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli zote za Halmashauri na miradi ya maendeleo.”

Muwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa ameongeza msisitizo kwa kusema, “Tusiposimamia usimamizi wa mapato haya yote tunayoyaomba hayatatimia.” Aidha, ameshauri fedha zielekezwe kwenye miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi. Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Bi Fatma Mohammed, amewapongeza madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo na kushauri kuongeza vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha utekelezaji wa miradi.

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Afisa Serikali za Mitaa Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Fabian Kamoga akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani humo cha kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 54.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Februari 12,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kishapu, Ndg. Emmanuel Johnson, amewapongeza wataalamu wa Halmashauri kwa kuandaa bajeti hiyo kwa weledi na kuwakumbusha madiwani kuhakikisha watoto wa shule ya awali na kidato cha kwanza waanaandikishwa na kuanza masomo vilevile, kushiriki katika hatua za awali za uhamasishaji wa bima ya afya kwa wote na utambuzi wa kaya zisizo na uwezo ili kuingia kwenye mpango wa kugharamiwa na Serikali.

Katika kikao hicho, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Elia Mgaya, amewasilisha mpango wa bajeti ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Waheshimiwa Madiwani wameweka azimio la kuomba fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya barabara, wakisisitiza kuwa barabara bora ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Wilayani humo.

Kupitishwa kwa bajeti ya bilioni 54.3 ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Utekelezaji wake unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali hususan miradi ya maendeleo na miundombinu ya barabara, na hivyo kuboresha maisha ya wananchi wa Kishapu.



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson (alievaa shati la draft) akifuatilia kwa makini kikao cha baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya hiyo cha kupitisha bajeti ya shilingi bilioni 54.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Februari 12,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa