
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi akikabidhiwa dawati na watumishi toka Benki ya CRDB Julai 28,2025
Wanafunzi 120 kutoka Shule za Msingi Mwakolomwa Kata ya Seke bugoro na Ndoleleji Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wamenufaika na msaada wa madawati 120 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 8 kutoka Benki ya CRDB, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uwajibikaji kwa jamii ya 1% ya faida ya benki hiyo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Julai 28,2025 katika shule ya Msingi Mwakolomwa na Ndoleleji Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi ameipongeza CRDB kwa moyo wa kujitoa kusaidia maendeleo ya elimu Wilayani humo.
"Nawashukuru CRDB kwa moyo wenu wa kizalendo mnaoonesha kuwa mnawekeza si tu kwenye biashara, bali pia kwenye ndoto za watoto wetu hivyo wazazi tuache kukatisha ndoto za watoto wetu kwa kuwaoza au kuwapeleka kuchunga mifugo badala ya kuwapa nafasi wasome" amesema Masindi

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe Peter Masindi
Mhe.Masindi amewahimiza wanafunzi kutenga muda wa kusoma na kuwa na nidhamu kwani ndiyo zawadi na amana kubwa katika maisha ya shule na baada ya shule

"Msingi mnaopewa ni kwa maisha na faida yenu pekee acheni utoro,jisomeeni na kuelekezana Ninyi kwa Ninyi,msiwe wabinafsi kwenye masomo hakuna aliyefanikiwa bila kusoma wakati huo muwatii na wazazi wenu" amesema Masindi
Amewataka waalimu kuongeza juhudi na kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
"CRDB wameonesha upekee wa kuwajali watoto wetu na nyie wazazi msiwafanye watoto ni vitega uchumi majumbani kwenu hasa wa kike na hao sio wachungaji wa mifugo mliyonayo wapeni nafasi wasome na mwahimize kwenda shule na kufanya vizuri ili baadae wawe msaada kwenu" Ameongeza Mkuu wa Wilaya huyo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa CRDB Bank Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Malipo CRDB Makao makuu Bw.Madaha Chabba ameishukuru Serikali ya Wilaya kwa ushirikiano mkubwa na moyo wa kupokea na kuthamini mchango wa taasisi binafsi kama CRDB.
"Serikali yenu imetupokea kwa moyo mmoja na kutambua thamani ya ushirikiano wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo," amesema Chabba.
Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi Bw. Jumanne Wagana amesema benki hiyo ina utaratibu wa kurejesha asilimia moja (1%) ya faida yake kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo hususa katika sekta za elimu, afya na mazingira.
"Tumekabidhi madawati haya 120 kwa shule mbili zenye changamoto kubwa ya miundombinu tunatambua kuwa mazingira bora ya kusomea ni msingi wa mafanikio ya mtoto wa Kitanzania," ameeleza Wagana.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Bi. Fatma Haji Mohamed, amewasisitiza wanafunzi kuyatunza madawati hayo na kuyatumia kwa ufanisi kama sehemu ya kujenga nidhamu na uthubutu wa kutimiza ndoto zao.
Wananchi na wazazi walioudhuria hafla hiyo wameonesha furaha na kuipongeza CRDB kwa msaada huo muhimu, wakisema utapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza ufanisi katika ujifunzaji.
"Mwenyezi Mungu aibariki CRDB Mtoto wangu alikuwa anakalia mawe na hata kukaa chini anarudi amechafuka sana lakini sasa atakalia dawati kama wengine." amesema mzazi Bunoge Nkinga.
Mwanafunzi wa dalasa la saba shule ya msingi Mwakolomwa Jackline Richard amesema sasa wanauhakika wa mazingira salama ya kujifunzia na kuandika.
Katika taarifa ya shule, Mwakolomwa iliyoko kata ya Sekebugoro imebakiwa na upungufu wa madawati 16 Kwa upande wa Shule ya Msingi Ndoleleji ikiwa na upungufu wa madawati 103 ambapo kila shule wamepokea madawati 60 kutoka CRDB, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.
Hii ni hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunza kwa watoto wa Kishapu, na ni mfano wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali katika kuinua elimu nchini.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa