Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi, ametoa wito kwa wananchi waliopokea mbegu zilizobarikiwa katika kilele cha Tamasha la Utamaduni wa Kisukuma "Sanjo ya Busiya", kuzitumia kwa tija katika msimu ujao wa kilimo ili kuboresha maisha na uchumi wa familia zao.
Akihutubia maelfu ya wakazi waliohudhuria tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Busiya – Ukenyenge Julai 7,2025 Mhe. Masindi amesema matumizi sahihi ya mbegu hizo ni msingi wa mafanikio kwa familia na jamii kwa ujumla.
"Wote mtakaochukua mbegu hizi zilizobarikiwa hakikisheni mnalima kwa wingi. Baada ya mavuno, watoto wasome, familia zinufaike. La sivyo, mkiziingiza kwenye matumizi ya anasa, fedha hizo zitageuka kuwa laana badala ya baraka," ameonya Mhe. Masindi.

MKuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe Peter Masindi (kulia) akizungumza na wananchi kwenye sherehe za Tamasha la Utamaduni la Sanjo ya Busiya kwenye viwanja vya Ikulu ya Busiya Ukenyenge Wilayani humo Julai 7,2025
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, maarufu kwa jina la heshima Chifu Hangaya, itaendelea kuhimiza jamii kuenzi na kulinda tamaduni njema kama sehemu ya urithi na maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika tamasha hilo, Mtemi Faustine Makwaia wa III wa Utemi wa Busiya, unaojumuisha kata kumi za Wilaya ya Kishapu amesisitiza kuwa upendo ni silaha muhimu ya kuleta maendeleo na kuondoa chuki katika jamii.
"Tukiwa na upendo ndipo maendeleo yatakuwepo. Kinyume cha upendo ni chuki, na pale panapokuwepo chuki hakuna maendeleo kwa kuwa hakuna maono ya pamoja.Amesema Makwaia wa III
Tamasha la Sanjo ya Busiya limejumuisha mashindano ya ngoma na muziki wa asili kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Kishapu, maonesho ya vyakula vya jadi vya Kisukuma, mavazi ya asili, na matumizi ya vyombo vya kijadi. Mgeni rasmi, Mtemi Makwaia wa III, alikabidhi zawadi kwa vikundi vilivyoshiriki, wanawake waliotoa mchango mkubwa katika mavazi na mapishi ya asili, na watoa huduma mbalimbali wa kitamaduni.

Mtemi wa Busiya Chifu Faustine Makwaia wa III Utemi wenye makao yake makuu Ukenyenge Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga akizungumza na wananchi kwenye sherehe za tamasha la Sanjo ya Busiya Julai 7,2025
Kwa ujumla, tamasha hilo limeonyesha mshikamano wa jamii, kuenzi mila na desturi za Kisukuma, pamoja na kuhimiza matumizi ya rasilimali za asili kwa maendeleo endelevu.

Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa