Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi ambaye pia ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa zoezi la chanjo Wilayani humo, amezindua rasmi kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha afya ya mifugo na kuongeza ushindani wa sekta hiyo nchini Tanzania.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi akiwa sehemu ya zoezi la utoaji chanjo kwa ng'ombe
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika kata ya Mwamashele, Mhe. Masindi amesema kampeni hiyo inatekelezwa kwa msaada wa ruzuku ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na inalenga kulinda ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku dhidi ya magonjwa hatari, sambamba na kuitambua rasmi mifugo hiyo kitaifa.
Kupitia ruzuku hiyo, chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe inatolewa kwa shilingi 500 tu, ikiwa ni nusu ya bei ya kawaida. Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Sotoka kwa mbuzi na kondoo zinatolewa kwa shilingi 300 badala ya 600, huku hereni za utambuzi zikitolewa bila malipo.

Mratibu wa zoezi hilo Wilaya ya Kishapu, Bw. John Mchele, amesema wamepokea chanjo 450,000 dhidi ya homa ya mapafu kwa ng’ombe na chanjo 442,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka kwa mbuzi na kondoo.

Mratibu wa chanjo ya mifugo Wilaya ya Kishapu Bw. John Mchele
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Mwita Mwijarubi Mwita, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu, ameeleza kuwa kampeni ya awali ya chanjo kwa kuku imefikia asilimia 87 ya utekelezaji. “Chanjo ni bure, na mwitikio umekuwa mzuri sana,” amesema.

Mkuu wa idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bw. Mwita .M. Mwita
Mhe. Masindi amewasihi wafugaji wote kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo ili kusaidia Serikali kuboresha huduma za mifugo ikiwemo upatikanaji wa dawa za mifugo, malisho bora na fursa za masoko kitaifa na kimataifa. “Tujitahidi wote, hakuna haja ya mtu kuficha ng’ombe wake. Ukificha mifugo wasiende kuchanjwa, unaficha takwimu zinazosaidia serikali kuboresha ustawi wa wafugaji,” amesisitiza.

Mhe. Masindi akiwasihi wananchi kutoa ushirikiano kwenye zoezi la utoaji wa chanjo ya mifugo yao
Aidha, wananchi wa Kata ya Mwamashele, wamepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya mifugo nchini, na kuahidi kutoa ushirikiano katika zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo. “Tunashukuru Serikali kwa kutuletea chanjo kwa bei nafuu, hii inalinda mifugo yetu na tunatarajia kukuza uchumi wetu,” Bw. Khalid Hamad .

Bw. Khalid Hamad, mfugaji na mkazi wa Kata ya Mwamashele


Kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kishapu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kuimarisha sekta ya mifugo kwa maendeleo endelevu ya jamii.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa