Shirika lisilo la kiserikali la HelpAge Tanzania limeendesha majadiliano ya makundi rika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, kwa lengo la kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza mila kandamizi, na kuimarisha afya ya uzazi, hususan kwa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu.

Tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu, unaofadhiliwa na Serikali ya Finland na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), kwa kushirikiana na wizara pamoja na taasisi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa mjadala huo, Mkuu wa Programu wa HelpAge Tanzania, Leonard Ndamgoba, alisema shirika hilo limeandaa mwongozo maalum wa majadiliano kati ya makundi ya wazee na vijana ili kukabiliana na changamoto zinazokumba jamii, hususan ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia.

"Kupitia mijadala ya makundi rika, tunatengeneza jukwaa la kuleta mabadiliko ya kweli kutoka kizazi kimoja kwenda kingine," alisema Ndamgoba na kuongeza kuwa wawezeshaji waliopatiwa mafunzo wataendesha mijadala hiyo katika mikutano ya hadhara, vikundi vya kijamii, na matukio ya kijamii kama misiba na harusi, huku wakijengewa uwezo wa kuendeleza juhudi hizo kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Ndamgoba, lengo ni kuvunja mitazamo potofu ya kijinsia kwa kujenga mazingira salama ya mazungumzo yanayowawezesha wanawake na wasichana, wakiwemo wenye ulemavu, kudai haki zao katika nyanja za elimu, uchumi, afya ya uzazi na ushiriki wa kijamii.

Naye Mratibu wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ibrahim Sakulia, alitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika hatua za utambuzi na utatuzi wa changamoto za ukatili na mila kandamizi.
“Tunahitaji wananchi washiriki kikamilifu mijadala hii kwa sababu wao ndio chachu ya mabadiliko tunayoyakusudia,” alisema Sakulia.

Katika mafunzo hayo, wawakilishi wa makundi ya vijana na wazee kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa na Mwamashele walipatiwa mbinu za kuendesha midahalo ya makundi rika katika maeneo yao, kwa lengo la kuchochea mijadala ya wazi kuhusu ukatili wa kijinsia, usawa wa kijinsia na heshima kwa haki za binadamu.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Hilda Ebunka, alisema hali ya mimba za utotoni imeanza kupungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo linaloashiria mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya serikali na mashirika ya kiraia.

Afisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri hiyo, Paul Lupolaso, alisema ofisi yake hupokea kesi nyingi za ukatili wa kijinsia, zikiwemo ndoa za utotoni, ukatili wa kimwili na unyanyasaji wa kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto.
"Ndoa za utotoni huwakosesha watoto haki ya elimu, afya bora na maendeleo ya baadaye," alibainisha Lupolaso.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Wilaya ya Kishapu, Inspekta Rose Mbwambo, alisema dawati hilo limekuwa msaada mkubwa kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, akihimiza jamii kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa na ushahidi mapema.

“Tunahitaji jamii kushirikiana nasi kwa ukaribu. Wananchi wafahamu kuwa kazi ya dawati letu ni kusaidia, siyo kuadhibu,” alisisitiza Inspekta Mbwambo.
Aidha, aliwasihi wazazi na walezi kuwafundisha watoto kuhusu haki zao na kuhakikisha wanawalinda dhidi ya ukatili wa aina yoyote.

Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao walisema kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa mapya kuhusu mbinu bora za kupambana na ukatili wa kijinsia, na wakaahidi kuyatumia katika jamii zao ili kuleta mabadiliko chanya.
HelpAge Tanzania inatarajia kuwa mwongozo wa mijadala ya makundi rika utachangia kuleta mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni kwa ajili ya kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia, heshima kwa haki za binadamu, na uhuru kwa kila mwanajamii – wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa