Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akikabidhi kishwambi kwa Afisa Mifugo wa Kata ya Uchunga.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amekabidhi vishkwambi 40 kwa maafisa mifugo Wilayani humo ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Septemba 26, 2025, Mhe. Masindi amewapongeza maafisa mifugo kwa kupokea vitendea kazi hivyo vya kidijitali, akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa hivyo katika ukusanyaji wa takwimu za mifugo.
“Serikali ya awamu ya sita inatambua mchango wenu na imewapatia vishkwambi hivi ili muweze kusaidia katika upatikanaji wa taarifa sahihi. Takwimu hizi ni msingi wa kupanga bajeti na mipango ya utoaji wa huduma kama vile dawa za mifugo hivyo, hakuna haja ya kuficha wala kuzembea kutoa taarifa” amesema Mhe. Masindi.
Ameongeza kuwa kupatiwa vitendea kazi ni ishara ya heshima na dhamana, hivyo ni wajibu wa kila Afisa kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa ufanisi na kwa kazi iliyokusudiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu akizungumza na Maafisa Mifugo wakati wa makabidhiano ya vishkwambi
Kwa upande wake, Mratibu wa chanjo na utambuzi wa mifugo Wilayani humo, John Mchele, ameeleza kuwa vishkwambi vinavyotolewa vitatumika kusajili mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo, ikiwa ni muendelezo wa juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya mifugo.

Mratibu wa chanjo na utambuzi wa mifugo Wilaya ya Kishapu, John Mchele akielezea dhumuni la kukabidhi vishkwambi kwa Maafisa Mifugo
Afisa Mifugo kutoka Kata ya Talaga, Juhudi Mwaluanda Anangisye ametoa shukrani kwa serikali na kuahidi kutumia kifaa chake kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Zamani tulikuwa tunatumia makaratasi, lakini sasa tunaenda kidijitali. Tunaahidi kuvitumia kwa usahihi ili kuboresha ustawi wa mifugo katika Wilaya ya Kishapu,” amesema Anangisye.

Afisa Mifugo wa Kata ya Talaga, Juhudi Mwaluanda Anangisye
Hatua hii inaashiria mwendelezo wa jitihada za serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mifugo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.



Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa