Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga, Bw. Joseph Sahani Swalala akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata Agosti 6,2025 katika Ukumbi wa Mwadui
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Bw. Joseph Sahani Swalala, amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata kuhakikisha wanazingatia maadili, uadilifu, na uwajibikaji mkubwa wakati wa kutekeleza majukumu yao katika kipindi chote cha uchaguzi.
Bw. Swalala ametoa wito huo leo Agosti 6, 2025, wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi hao, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwadui wilayani Kishapu. Amesema kuwa nafasi waliyopewa si ya kawaida bali ni dhamana kubwa ya kitaifa, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na kuzingatia misingi ya sheria, kanuni, na taratibu zinazosimamia uchaguzi.
"Ninyi sasa ni sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, dhamana mliyokabidhiwa ni kubwa. Msikubali kushawishika au kuingiliwa na mtu yeyote katika utekelezaji wa majukumu yenu fanyeni kazi kwa haki, usawa na kwa mujibu wa mafunzo haya," amesema Swalala.
Aidha, amewataka kuhakikisha kuwa wanatumia ujuzi walioupata kwa makini na kuwa kielelezo chema katika maeneo yao, akisisitiza kuwa uchaguzi ni mchakato nyeti unaohitaji usimamizi makini ili kudumisha amani na demokrasia nchini.
"Tumepewa jukumu hili kwa niaba ya wananchi na nchi Kwa hiyo hatuna budi kulitumikia kwa moyo wa uzalendo na kujituma, maadili ya kazi ya uchaguzi ni jambo lisilopaswa kupuuzwa hata kidogo," ameongeza.
Mafunzo yamelenga kuwaandaa wasimamizi wasaidizi kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, yakijikita katika maeneo muhimu kama sheria za uchaguzi, maadili ya watendaji, taratibu za upigaji kura na namna ya kushughulikia changamoto katika vituo vya kupigia kura.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wasimamizi kutoka kata zote za Wilaya ya Kishapu, huku washiriki wakionesha hamasa kubwa na utayari wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa